Monday, June 30, 2014

WAZIRI MKUU: MAANDALIZI YA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA YANAENDELEA

1(5) 
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao unatarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu yanaendelea japo kwa kiasi kikubwa hatma yake inategemea kukamilika kwa mchakato wa Katiba mpya.

Ametoa kauli hiyo leo  wakati akizungumza na Mameya wa Majiji, Manispaa na Wenyeviti wa Halmashauri za Miji na Wilaya Tanzania katika kikao cha siku moja kilichofanyika kwenye ukumbi wa Regal Naivera jijini Tanga.

Waziri Mkuu yuko Tanga kwa ajili ya sherehe za Serikali za Mitaa ambayo kilele chake kitafanyika kesho Julai mosi kwenye uwanja wa Tangamano jijini hapa. Ameamua kukutana na viongozi hao ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya kukutana nao aliyoitoa Mei 14, 2014 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa ALAT.

“Uchaguzi wa Serikali za Mitaa bado ni kitendawili kwa sababu kwa kiasi kikubwa inategemea sana kukamilika kwa Mchakato wa Bunge la Katiba,” alisema na kuongeza:
“Kama Wizara tunaendelea na maandalizi tukiamini uchaguzi upo, kama hiyo fursa isipotokea bado tutakuwa tumekamilisha maandalizi kwa upande wetu.Tunaendelea kuandaa kanuni kwa kushirikisha wadau wote,” alisema.

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kusisitiza suala la ukusanyaji mapato na udhibiti wa matumizi ya fedha za Serikali. Kuhusu mapato, Waziri Mkuu alisema katika mwaka wa fedha wa unaoisha sasa, hali ya ukusanyaji mapato haikuwa nzuri.
Kufuatia hali hiyo, Waziri Mkuu alisema amewaandikia barua Wakuu wa Mikoa akiwataka waweke utaratibu wa kutoa taarifa kila baada ya miezi mitatu juu ya makusanyo ya kila Halmashauri zilizo kwenye mikoa yao.

“Katika taarifa hizi itabidi kila Halmashauri ieleze ilipanga kukusanya kiasi gani, je imefikia lengo na kama sivyo ni kwa nini. Nia yetu ni kutrack down makusanyo na kuona yamekwama wapi na yamekwamishwa na nini,” alisema.

Kuhusu udhibiti wa matumizi, Waziri Mkuu aliwataka Mameya na Wenyeviti hao kuendelea kuwabana wahusika ili kudhibiti matumizi yasiyofaa. “Lazima muendelee kuwabana na kuwasimamia wakurugenzi na wataalaam wa kwenye Halmashauri zenu. Fanyeni kazi kwa ufanisi, msiwachekee wale wanaoharibu,” aliongeza.

“Ili muweze kuwabana vizuri, ni lazima mdai kupatiwa taarifa za fedha kutoka kwa Mkaguzi wa Ndani (Internal Auditor)… kuna baadhi ya watendaji wanadai kuwa hizi taarifa ni siri wakati siyo siri,” alisema.

Aliwaeleza washiriki wa kikao hicho kwamba taarifa hizo ni muhimu kwao kuzipata na zitawasaidia kuonyesha mapungufu yoyote kama yapo.
Aliwataka kila mmoja wao kwa nafasi zao za Meya na Mwenyekiti wahakikishe wanalenga kupandisha pato la wananchi wanaowaongoza.

No comments: