NA GRACE SHITUNDU
MWENYEKITI
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amepuuza
kauli na maagizo yaliyotolewa juzi na Msajili Msaidizi wa Vyama vya
Siasa nchini, Sisty Nyahoza.
Nyahoza
alinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari likiwemo gazeti hili kuwa
Mbowe hawezi kuongoza tena chama hicho kwa muhula mwingine hata kama
atashinda kwenye uchaguzi wa chama hicho.
Alisema
hatua hiyo inatokana na chama hicho kukiuka katiba yake kwa kubadilisha
kipengele cha ukomo wa uongozi kutoka ukomo wa mihula miwili hadi
kutokuwa na ukomo wa uongozi.
Nyahoza alisema kuwa mabadiliko hayo ya katiba hayakufuata taratibu stahiki, ikiwa ni pamoja na kutopata baraka za Mkutano Mkuu
...........................
Mbali na
suala hilo, Nyahoza pia aliutaka uongozi wa chama hicho kuhakikisha
Januari mwakani kinaitisha Mkutano Mkuu wa uchaguzi ili kuwapata
viongozi wapya.
Akijibu
kauli hizo jana, Mbowe alisema tamko lililotolewa na Msajili ni kituko
na kichekesho kwa kuwa ukomo wa uongozi wa chama hicho ni uamuzi na
utashi wa wanachama wenyewe.
Akizungumza
kwa simu ya mkononi na MTANZANIA Jumatano jana, Mbowe alisema chama cha
siasa kinaongozwa kwa demokrasia na kwamba ni utashi wa wanachama
wenyewe kuweka ukomo wa uongozi.
"Msajili
kuingilia mambo ya ndani yanayohusu ukomo wa uongozi wa chama mimi naita
ni kichekesho na ni kituko, huo ni uamuzi wa ndani ya chama na siyo
uamuzi wa Msajili.
"Chama
cha siasa sio sawa na Serikali, sisi tunaongozwa na demokrasia, suala la
katiba na kubadili baadhi ya vipengele ni la wanachama wenyewe ambao
ndio wanaamua katiba yao iweje, mabadiliko au uamuzi katika chama
unafanywa na wanachama katika vikao, inawezekana wachache wakayakataa
mabadiliko hayo lakini wengi wakayakubali, hivyo yanatakiwa
yaheshimiwe," alisema Mbowe.
Aliongeza
kuwa kila chama kina haki na mamlaka ya kuamua viongozi wao wakae muda
gani madarakani, ambapo wanaweza kuamua kukaa miaka 10 au zaidi.
Alisema
suala la yeye kuwania nafasi hiyo kwa mara nyingine ni suala binafsi
ambalo linatokana na utashi wake ikiwa ataamua kugombea au la!
Aidha
aliweka wazi kuwa sifa za kuwania nafasi hiyo kama katiba yao inavyotaka
anazo, ambapo pia anaamini wanachama wanautambua mchango wake ndani ya
chama katika kipindi chote alichokaa madarakani.
MNYIKA AMUONYA
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, John Mnyika,
alimuonya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kuacha kutangaza mgogoro na
Chadema.
Mnyika alisema anaamini Msajili anaingizwa kwenye mtego wa kutumika jambo ambalo linaweza kumuondolea sifa.
Akikosoa
kauli ya Nyahoza, Mnyika alisema Msajili hana uwezo wa kumzuia Mbowe ama
mwanachama yeyote wa chama hicho kuwania uongozi na kwamba chama chao
hakiongozwi na matamko ya watu.
Alisema
chama chao hakijakiuka kipengele chochote cha katiba wanayoitumia sasa,
ambayo waliiboresha zaidi kwenye Mkutano Mkuu wa chama hicho uliofanyika
Agosti 13, 2006.
Alisema
Mkutano Mkuu wa mwaka 2006 ulitumika kuboresha katiba, bendera, kadi
pamoja na kuweka mikakati na mipango ya chama na kwamba mkutano huo
uliidhinisha mabadiliko yote.
Mnyika
aliongeza kuwa katiba yao ya mwaka 2006 kifungu cha 6.2 (c) kinatoa
mamlaka kwa kiongozi kuwania uongozi na kuchaguliwa endapo ametimiza
masharti yote.
"Ofisi ya
Msajili haina uwezo wa kumzuia Mbowe au mwanachama yeyote wa Chadema
kuwania uongozi kama ametimiza masharti, chama chetu kinaongozwa na
taratibu kwa kufuata katiba yake, tunamuomba msajili kutoingia kwenye
mtego wa kutumika.
"Akiendelea
kufanya haya aliyoanza kuyafanya atakuwa ametangaza mgogoro na sisi na
hatutamtambua kama ambavyo tulimfanyia mtangulizi wake, John Tendwa.
"Mwaka
2006 tuliandika katiba mpya, hata hivyo baadhi ya mambo ya katiba ya
zamani tuliyapa nafasi na kipengele cha ukomo wa uongozi kiliridhiwa na
Mkutano Mkuu baada ya kusambazwa kwa waraka wa mabadiliko ya katiba nchi
nzima na mapendekezo yalifikishwa kwenye ngazi zote husika kabla ya
kufikishwa kwenye Mkutano Mkuu ambao nao uliridhia," alisema.
Aidha
alisema kinachoendelea sasa hivi ni mikakati ya baadhi ya watu ndani na
nje ya chama chao kuhakikisha wanawapindua viongozi wa juu wa chama
hicho.
"Upo
msemo unaosema, mpige mchungaji kondoo watatawanyika, tumeshazibaini
mbinu zao, wameshindwa kwenye waraka wa mabadiliko, wameshindwa kwenye
kuwachafua viongozi wetu sasa wanaitumia ofisi ya Msajili wa Vyama,
nawahakikishia wahusika wa uovu huu hawatafanikiwa," alisisitiza Mnyika.
Mnyika
alikwenda mbali zaidi kwa kumtaka Msajili wa Vyama Vya Siasa, Jaji
Francis Mutungi, kujitokeza hadharani na kuzitolea ufafanuzi kauli
zilizotolewa na msaidizi wake.
Alihitimisha
kwa kusema kuwa ofisi ya Msajili isiwafundishe kazi kwani suala la
kufanya ama kutokufanya uchaguzi ni la chama na kwamba mipango yao ni
kufanya uchaguzi mwaka huu na si mwakani kama Nyahoza alivyotaka.
"Mwezi
huu tutaanza uchaguzi wa viongozi wa majimbo na wilaya, mwezi Agosti
tutafanya chaguzi za mikoa na mwezi Septemba tutafanya uchaguzi wa ngazi
ya taifa, asitufundishe kazi na aepuke kutangaza mgogoro na sisi, kama
hajui akamuulize Tendwa," alihitimisha Mnyika.
Nyahoza
katika mazungumzo yake na waandishi wa habari juzi alisema vyama vyote
vya siasa nchini vinaongozwa na kufuata katiba walizojiwekea wenyewe.
Alisema
ofisi ya msajili inafanya kazi kisheria ikiwa ni pamoja na kusimamia
katiba za vyama hivyo na kutoa mwongozo na kwamba kama kuna baadhi ya
vyama vinakwenda kinyume na katiba yake, ofisi hiyo inalazimika
kuingilia kati.
No comments:
Post a Comment