Wednesday, July 2, 2014

Mwigamba: Sikuwa kichaa

Samson Mwigamba
Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba

NA ELIYA MBONEA, ARUSHA

ALIYEWAHI kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, amesema hakuwa kichaa wala punguani wakati alipopeleka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa malalamiko ya kuvunja Katiba ya chama hicho kwa kubadili kipengele cha Katiba kilichoondoa ukomo wa uongozi.(Martha Magessa)

Mwigamba, ambaye kwa sasa ni Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha ACT- Tanzania, alimshukuru Mungu kwa Ofisi ya Msajili kusimamia na kuwaeleza ukweli wanachama wa Chadema juu ya alichokiwasilisha.
"Unajua wakati napiga kelele ndani ya chama baadhi ya viongozi na wanachama wa Chadema waliniona mimi kama kichaa na punguani. Wakaamua kunivua uongozi na uanachama.

"Ni wakati muafaka sasa kwa wanachama wao kutambua kuwa nilikuwa napigania mambo ninayoyajua, sikuwa kichaa kama walivyodhani na kuamua kunitukana na kunidharau," alisema Mwigamba.

Mwigamba alikwenda mbali na kufananisha kombora alilowapiga Chadema kuwa ni sawa na la kivita ambalo hurushwa na kuishambulia ndege kila inakoelekea na hatimaye kuidondosha.
Alisema katika mazingira ya kutokuelewa, Chadema walimfukuza uanachama wakiamini kwamba hoja ya kuvunja katiba ya chama aliyokuwa ameiwasilisha kwa ofisi hiyo ya msajili ingetupwa.

"Baada ya wao kunifukuza uanachama kwa kweli sikufuatilia tena hoja niliyokuwa nimeipeleka Ofisi ya Msajili kwa sababu nilijua sipo huko na tayari nilikuwa naendelea na mambo yangu mengine.
"Lakini cha ajabu kumbe msajili aliona hoja niliyoipeleka ilikuwa na mashiko na ndiyo maana aliendelea kuifanyia kazi na hatimaye amejiridhisha kuwa Chadema walikuwa wamevunja katiba ya chama chao," alisema.
CHANZA:MTANZANIA
Post a Comment