*Ujenzi kugharimu USD bilioni saba
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema
Serikali ina mpango wa kujenga reli mpya ya kutoka Dar es Salaam hadi
Mwanza kupitia mikoa na ya kati na kuelekea Isaka hadi Burundi ambayo
ujenzi wake utazinduliwa rasmi Desemba, mwaka huu
Ametoa kauli hiyo jana jioni
(Alhamisi, Julai 10, 2014) wakati akijibu maswali kutoka kwa Watanzania
waishio Reading katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa hoteli ya
Crowne Plaza.
Waziri Mkuu ambaye alitumia
usafiri wa treni kwenda na kurudi mji wa Reading kutoka London, alisema
ni mara yake ya kwanza kufika kwenye mji huo na akaahidi katika siku za
usoni kufanya mikutano ya aina hiyo kwa Watanzania waishio kwenye miji
mingine ya Uingereza kulingana na ratiba ambayo watu wa ubalozini
watakuwa wameipanga.
“Kuna mtu ameulizia kuhusu tatizo
la usafiri nchini Tanzania, napenda kuwahakikishia kwamba Serikali
imeamua kuwekeza kwenye mradi mkubwa wa ujenzi wa reli ya kati. Reli hii
itaanzia Dar es Salaam hadi Isaka, Isaka hadi Burundi; itatokea Tabora
hadi Kigoma na Tabora hadi Mwanza pamoja na kipande cha Kaliua hadi
Mpanda,” alisema.
“Mradi huu ni mkubwa ambao ujenzi
wake utagharimu dola za marekani bilioni saba, na utatuchukua karibu
miaka minne. Kwa hiyo ikiifika Desemba, mwaka huu utafanyika uzinduzi
rasmi kwa njia zote hizi za reli,” alisisitiza Waziri Mkuu.
Alisema ili kufanikisha ujenzi Serikali imeamua kujenga upya reli ya kati kwa standard gauge haliambayo
haitaathiri usafiri wa treni kwa kutumia njia ya zamani. “Safari hii
tumeamua kujenga upya, na siyo kubanduabandua ili wakati reli mpya
ikiendelea kujengwa na ile ya zamani inaendelea kutoa huduma kama
kawaida,” alisema huku akishangiliwa.
Maswali mengine aliyoulizwa Waziri
Mkuu yalihusu ujenzi wa barabara ya Lindi-Mtwara, ujenzi wa hospitali
ya Kagwa, ujenzi wa uwanja wa ndege wa Musoma, utaratibu wa utoaji wa
mizigo bandarini na usumbufu wanaoupata, uraia wa nchi mbili, tatizo la
walimu na hali ya elimu nchini ambayo yote aliyajibu na kuahidi
kufuatilia masuala mengine akifika nyumbani
Kwa ujumal, Waziri Mkuu aliwataka
Watanzania waishio nchi za nje (wana Diaspora) kufuatilia kwa makini
mikutano ya uwekezaji (Investors’ Forums) ambayo hufanyika kwa kanda au
kwa mikoa ili iwasadie kubaini fursa za uwekezaji zilizoko kwenye mikoa
wanayotoka. “Tumieni fursa hizi, zitawasaidieni kubaini kwa haraka ni
maeneo gani mnaweza kuwekeza kwa haraka. Kama Diaspora mnaweza pia
kutumia kipengele cha utalii wa Tanzania kutusaidia kuitangaza nchi
yetu,” alisema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu kesho jioni (Jumamosi,
Julai 12, 2014) anatarajiwa kukutana na Watanzania waishio Uingereza
kwenye mkutano utakaofanyika kwenye ubalozi wa Tanzania, jijini London.
No comments:
Post a Comment