Friday, November 28, 2014

MAELEZO YA SERIKALI KUHUSU TAARIFA YA UKAGUZI MAALUM KUHUSIANA NA MIAMALA ILIYOFANYIKA KATIKA AKAUNTI YA “ESCROW” YA TEGETA PAMOJA NA UMILIKI WA KAMPUNI YA IPTL

unnamed1
1.  Historia ya Mradi
 
Mheshimiwa Spika, Katika miaka ya tisini (1990s), Tanzania ilikuwa ikikabiliwa na tatizo la uhaba wa maji katika mabwawa ya kuzalisha umeme, hali iliyopelekea kuwepo kwa upungufu wa umeme na kuathiri shughuli za maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini. Ili kukabiliana na tatizo hilo, Serikali ilichukua hatua za dharura za kuanzisha mradi wa kufua umeme wenye uwezo wa kuzalisha Megawati (MW) 100.
 
2.  Upatikanaji wa IPTL
 
Mheshimiwa Spika, Mwaka 1994 Serikali ilitoa kazi ya uwekezaji kwa Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) iliyokuwa inamilikiwa na Kampuni za VIP Engineering and Marketing Ltd ya Tanzania iliyokuwa na Asilimia 30 na MECHMAR Corporation ya Malaysia (MECHMAR) iliyokuwa na Asilimia 70. Kampuni ya IPTL ilipewa leseni ya kujenga, kumiliki na kuendesha (Build-Own-Operate) Mtambo wenye uwezo wa kuzalisha umeme wa MW 100 kwa kutumia mafuta mazito eneo la Tegeta-Salasala, Dar es Salaam.
 
Katika Ukurasa wa 52 Aya ya 2 ya Taarifa ya PAC, Kamati imependekeza Mtambo huo utaifishwe.
 
Ufafanuzi:
 
Mheshimiwa Spika, Kulingana na Mkataba wa PPA kati ya TANESCO na IPTL, majukumu ya IPTL yalikuwa ni kujenga, kumiliki na kuendesha (Build, Own and Operate – BOO). Hivyo, kutaifisha Mtambo huo ni kukiuka makubaliano katika Mkataba wa PPA wa tarehe 26 Mei 1995, ukiukwaji wa aina hii ukitokea unaweza kuingiza Serikali katika mgogoro mkubwa ikiwa ni pamoja na kushtakiwa kwenye Mahakama za kibiashara za kimataifa. Aidha utaifishaji wa miradi ya uwekezaji binafsi itakuwa ni njia ya kufukuza wawekezaji binafsi.
 
Mheshimiwa Spika, Tarehe 26 Mei, 1995, TANESCO na IPTL walisaini Mkataba wa PPA kwa muda wa miaka ishirini (20), kwa ajili ya kununua umeme utakaozalishwa na IPTL. Kwa mujibu wa Mkataba huo, IPTL ilitakiwa kuiuzia TANESCO umeme usiopungua Asilimia 85 ya uwezo wa Mtambo (minimum off take). Hata hivyo, uzalishaji wa umeme haukuanza mara moja kutokana na mgogoro uliotokea kati ya TANESCO na IPTL kuhusu gharama halisi za uwekezaji na namna ya kukokotoa Capacity Charges. Hivyo, IPTL ilianza kuzalisha umeme tarehe 15 Januari, 2002. Kutokana na hali hiyo muda wa miaka 20 ya Mkataba ulianza kuhesabiwa tarehe 15 Januari, 2002 baada ya kuanza uzalishaji (Commercial Operation Date).
 
Mheshimiwa Spika, Pamoja na mambo mengine muhimu yaliyokuwemo katika PPA, Kifungu Na. 6 cha Mkataba huo kinaipa TANESCO wajibu wa kulipa malipo yaliyotajwa hapo juu na kwamba endapo kutakuwa na mgogoro wowote kuhusiana na malipo hayo (Disputed Amount), itafunguliwa Akaunti maalum (Escrow Account) ya kuhifadhi fedha hizo hadi pale pande mbili zitakapokubaliana juu ya uhalali wa malipo yanayobishaniwa. Aidha chini ya PPA, migogoro yote kuhusiana na masuala ya utekelezaji wa Mkataba huo ilitakiwa kuwasilishwa na kuamuliwa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID) ya London. Hivyo, ilikuwa ni jukumu la kila mhusika katika Mkataba huu kuwasilisha malalamiko yake ICSID yanapotokea.
 
 
 
Katika Ukurasa wa 8 Aya ya 2 ya Taarifa ya PAC imeelezwa kuwa mwaka 2004 TANESCO ilifungua shauri la ICSID 2 kupinga kiasi kikubwa cha tozo ya Capacity Charge.
 
Ufafanuzi
 
Mheshimiwa Spika, Taarifa hiyo siyo kweli kwani TANESCO haijawahi kufungua shauri lolote ICSID ya London au Mahakama yo yote dhidi ya Standard Charterd Bank kupinga kiasi kikubwa cha Capacity Charge kama inavyoelezwa katika Taarifa ya PAC. Shauri la ICSID 2 lilifunguliwa tarehe 31 Oktoba 2010 na Standard Chatered Bank Hong Kong (SCBHK) kwa ajili ya kudai malipo ya deni ililonunua kutokana na mkopo uliotolewa na mabenki ya ushirika ya Malaysia kwa IPTL.  Wahusika katika Shauri hilo la ICSID 2 ni SCBHK na TANESCO na wala siyo TANESCO na IPTL.
 
Mheshimiwa Spika, Tarehe 12 Februari, 2014 ICSID ilitoa uamuzi kuhusiana na Shauri la SCBHK na TANESCO na kuwashauri wakae kukokotoa upya malipo ya Capacity Charge. Hata hivyo, ilikuwa vigumu kwa pande hizo kutekeleza uamuzi huo kutokana na pande hizo kutokuwa na Mkataba wa kibiashara baina yao. Vile vile, kupitia Shauri la Madai Na. 60/2014, lililofunguliwa Mahakama Kuu ya Tanzania na IPTL tarehe 4 Aprili, 2014 ilizuia utekelezaji wa maelekezo hayo.
 
3.  Mgogoro kati ya IPTL na TANESCO
 
Mheshimiwa Spika, Migogoro kati ya TANESCO na IPTL ilianza muda mfupi baada ya PPA kusainiwa tarehe 26 Mei 1995. IPTL waliitaka TANESCO wakubaliane bei za kununua umeme kwa kuzingatia gharama za uwekezaji. Pande hizo mbili zilishindwa kukubaliana gharama za Capacity Charge kwa vile TANESCO walidai kuwa gharama zilizoainishwa na IPTL ni kubwa kuliko gharama halisi za uwekezaji. Mwaka 1998, TANESCO iliajiri Kampuni ya Mawakili ya Mkono & Co Advocates kutoa huduma za kisheria kwa kushirikiana na Huntons & Williams ya Marekani. Kutokana na tofauti za gharama za Uwekezaji, Mawakili hawa waliishauri TANESCO ifungue Kesi ICSID nchini Uingereza dhidi ya IPTL ili kupinga gharama hizo.
 
Mheshimiwa Spika, Kwa kuzingatia ushauri huo wa Mawakili, TANESCO ilifungua Kesi Na.ARB/98/8 ya mwezi Agosti, 1998 ikidai kuwa gharama halisi za uwekezaji ni Dola za Marekani milioni 90 na siyo milioni 163.53 kama ilivyodaiwa na IPTL. Aidha, IPTL ilidai kuwa kiwango cha marejesho ya uwekezaji (Internal Rate of Return-IRR) ni Asilimia 23.10 ambacho pia kilipingwa na TANESCO.
 
Mheshimiwa Spika, Tarehe 12 Julai, 2001, ICSID ilitoa uamuzi wa Kesi hiyo pamoja na mambo mengine kwamba:-
 
i.     Gharama halisi za uwekezaji zikiwemo Mtambo na nyumba za wafanyakazi wa IPTL zilizoainishwa katika hesabu ya IPTL zilikuwa ni Dola za Marekani milioni 163.53 lakini ICSID iliona kuwa gharama halisi ni Dola za Marekani milioni 127.20;
 
ii.     Kiwango cha marejesho ya uwekezaji (Internal Rate of Return-IRR) ilikuwa Asilimia 22.31 badala ya Asilimia 23.10 iliyodaiwa na IPTL; na
iii.  TANESCO na IPTL wakubaliane mfumo wa malipo ya kununua umeme ukizingatia gharama halisi za uwekezaji na kiwango cha marejesho ya uwekezaji (IRR) cha Asilimia 22.31 kwa kutumia financial model iliyokubalika na ICSID.
 
Katika Ukurasa wa 11 Aya ya 2 ya Taarifa ya PAC, imeelezwa kuwa mtaji wa uwekezaji katika Mtambo wa IPTL ni Shilingi 50,000/= na kwamba huo ndio ungetumika kukokotoa Capacity Charges ili kulipa tozo ndogo kuliko ilivyo sasa.
 
Ufafanuzi
 
Mheshimiwa Spika, Maelezo hayo siyo sahihi. Ukweli ni kwamba kutokana na maamuzi ya ICSID 1 ya tarehe 12 Julai, 2001, gharama za ujenzi wa Mtambo wa Tegeta ni Dola za Marekani 127.20 kama ilivyoelezwa katika Ukurasa wa 47 Aya ya 4 ya Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Katika Taarifa hiyo, pia imeelezwa kuwa ilikubalika kuwa uwiano wa deni na mtaji utakuwa 70:30. Hii ikiwa na maana kwamba, deni ni Dola za Marekani milioni 89.04 na mtaji ni Dola za Marekani milioni 38.16. Uamuzi huo haujabadilishwa na Mahakama yo yote au mtu ye yote.
 
Mheshimiwa Spika, Tunakubaliana kwamba fedha iliyopokelewa kutoka Mabenki ya Ushirika ya Malaysia kama mkopo ni Dola za Marekani milioni 85.86 ambazo kati ya Dola za Marekani milioni 105 zilizokuwa zimeidhinishwa. Swali la kujiuliza, je Mtambo huo ulikamilikaje kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 85.86, huku gharama halisi ya ujenzi wa Mtambo wa Tegeta ikawa Dola za Marekani milioni 127.20?
 
Mheshimiwa Spika, Ni dhahiri kwamba kuna matumizi ya zaidi ya Dola za Marekani milioni 38.16 ambazo pia zimetumika kwenye uwekezaji. Taarifa ya Kamati ya PAC haikuonesha fedha hiyo kuwa sehemu ya uwekezaji.
                                        
Mheshimiwa Spika, Tarehe 30 Juni, 2004, Kampuni ya Mawakili iliyokuwa ikiiwakilisha TANESCO katika kesi ya kwanza ya usuluhishi, Kampuni ya Mkono & Co Advocates, iliishauri TANESCO iendelee kupinga kiwango cha malipo ya Capacity Charge kilichokuwa kimeafikiwa tarehe 12 Julai, 2001 na pande hizi mbili katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICSID) ya London. Hii ilikuwa ni miaka miwili tu baada ya usuluhishi uliochukua miaka minne kukamilika na Mtambo kuanza kuzalisha umeme tarehe 15 Januari, 2002.
 
Mheshimiwa Spika, Hata hivyo, baada ya ushauri huu, Mawakili hawa (Mkono & Co. Advocates) hawakuishauri TANESCO ifungue kesi katika Mahakama za Tanzania wala katika Mahakama ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kimataifa (ICSID) ya London.
 
Mheshimiwa Spika, Hadi kufikia tarehe 5 Septemba, 2013 wakati Mheshimiwa Jaji Utamwa anatoa hukumu yake juu ya mgogoro wa Wanahisa wa IPTL hapakuwepo na kesi yo yote kwenye Mahakama yo yote ya kupinga gharama za Capacity Charge kati ya TANESCO na IPTL, iwe katika Mahakama za ndani au za nje. Kwa kutokuwepo Msuluhishi (Broker) katika suala hili, madai yo yote ya TANESCO yanakuwa ni madai ya upande mmoja ambayo kisheria hayawezi kuchukuliwa kuwa ndiyo madai halisi.  Kwa sababu hiyo haikuwepo formula rasmi ya kuutatua mgogoro huo zaidi ya majadiliano na maafikiano kati ya pande mbili (TANESCO na IPTL).
 
4.  Uuzaji wa Hisa za VIP
 
Continue reading →

MATUKIO YA PICHA KUTOKA BUNGENI DODOMA

unnamed 
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma Novemba 27, 2014.
unnamed3 
Spika wa Bunge Anne Makinda akizungumza, Bungeni Mjini Dodoma Novemba 27, 2014.
unnamed5 
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma Novemba 27, 2014.
unnamed8
Waziri  Mizengo Pinda  akizungumza na Mbunge wa Maswa Magaribi, John Cheyo, kwenye viwanja vya Bunge Mjini Dodoma Novemba 27, 2014. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) unnamed10 
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiteta na Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole- Sendeka kwenye viwanja vya Bunge Mjini Dodoma Novemba 27, 2014. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) unnamed11 
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe (katikati) na Mbunge wa Lshoto, Henry Shekifu kwenye jengo la Utawala la  Bunge mjini Dodoma Novemba 27, 2013. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Post a Comment