Monday, December 8, 2014

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUTOKA MAKAO MAKUU YA JESHI LA POLISI

Advera-Senso
Tunapoelekea kipindi hiki cha uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ambao unatarajiwa kufanyika tarehe 14 Disemba, 2014, kwa taarifa tulizonazo, katika baadhi ya maeneo hapa nchini, kumejitokeza makundi ya vijana wanaopita katika baadhi ya maeneo na kuwatishia watu waliojiandikisha kupiga kura hususani wazee na wanawake kuwa, siku ya kupiga kura wasijitokeze na endapo watajitokeza watafanyiwa vurugu.
Jeshi la Polisi nchini, linatoa onyo kali kwa mtu yeyote au kikundi chochote cha watu kutokujihusisha na vitendo vya vurugu, fujo ama vitisho vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani wakati wa zoezi zima la uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi katika mikoa yote limejipanga vizuri kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuhakikisha kwamba hakuna vitendo vyovyote vya uvunjifu wa amani vitakavyojitokeza wakati wa kampeni na hata siku ya kupiga kura na pale ambapo vitajitokeza vitadhibitiwa kwa haraka, na wahusika kukamatwa.
Aidha, Jeshi la Polisi nchini, linawatoa hofu wananchi wote kwamba, ulinzi umeimarishwa katika maeneo yote kipindi hiki chote cha kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa na hata siku ya upigaji kura. Waliojiandikisha kupiga kura wote wajitokeze siku ya kupiga kura bila hofu ya aina yoyote.
Jeshi la Polisi linaendelea kuomba ushirikiano wa jamii kutoa taarifa za mtu ama vikundi vya aina yoyote vinavyojihusisha na vitendo vya vitisho, vurugu na fujo dhidi ya wananchi waliojiandikisha kupiga kura ili hatua kali za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao mapema.
Imetolewa na:-
Advera John Bulimba – SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.
Post a Comment