Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Jumanne Sagini
SERIKALI
imesema ajira za walimu wapya zitaanza rasmi Mei Mosi, mwaka huu huku
ikiweka wazi kuwa walimu hao wasitegemee kupangiwa katika maeneo ya
majiji, manispaa na miji.
Walimu
hao wametakiwa kutotegemea kupangiwa katika maeneo hayo kutokana na
idadi ya walimu waliopo ni kubwa na inakidhi mahitaji, huku maeneo
yaliyopewa kipaumbele ni vijijini na halmashauri ambazo zina mahitaji na
upungufu mkubwa wa walimu.
Idadi ya
walimu wapya watakaoanza ajira zao mwezi ujao ni 31,056 ambapo kwa
walimu wa ngazi ya Cheti ni 11,795, Stashahada (Diploma) 6,596 na wenye
Shahada (Degree) 12,665.
Hayo
yameelezwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Jumanne Sagini wakati akizungumza na
waandishi wa habari kuhusu ajira mpya za walimu kwa mwaka 2014/2015.
Alisema
kwa mwaka huu ajira hizo zimechelewa kutokana na TAMISEMI pamoja na
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kufanya ufuatiliaji wa kina hadi
katika ngazi ya shule ili kubaini kwa uhakika mahitaji halisi ya walimu
kwa kila halmahauri na shule.
“Ufuatiliaji
huo umebaini kuwepo kwa halmashauri na shule hasa za mjini zenye walimu
wa ziada na zingine hasa za vijijini zina upungufu mkubwa wa walimu,”
alisema Sagini.
Alisema
taarifa hizo zimesaidia kuwapanga walimu wapya kwa usawa ili kuondoa
uwiano usioridhisha kwenye maeneo mengi ya vijijini. Alisema kwa sasa
wanakamilisha taratibu za kupata kibali kwa ajili ya ajira za walimu na
fedha za kuwalipa stahili zao ili waanze ajira zao rasmi mwezi ujao.
Aidha,
alisema orodha ya walimu na vituo watakavyopangiwa vitawekwa katika
tovuti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI ambayo ni www.pmoralg.com na ya
Wizara ya Elimu www.moe. go.tz ifikapo Aprili 24, mwaka huu.
Kwa
upande wake Naibu Katibu Mkuu wa TAMISEMI, Zuberi Samataba alisema, pia
ufuatiliaji huo ulikuwa ni kuhakikisha wanakuwa na taarifa sahihi za
walimu wanaoajiri wote ni wapya ambao hawajawahi kuajiriwa ili kuepuka
usumbufu kwa walimu ambao hawatoi taarifa.
Alisema
baadhi ya walimu ambao wameshaajiriwa wanapoenda kusoma, hupangiwa upya
vituo na hawatoi taarifa hivyo kuleta usumbufu wa kuchelewa kutopata
mishahara yao.
“Kuna
baadhi ya walimu wameshaajiriwa kwa hiyo jina linapoingizwa katika
taratibu za malipo, linagoma kuingia ndipo ukifuatilia unajua alikuwa
ameajiriwa, inabidi umwambie arudi kwa mwajiri wake.
Kwa hiyo
kwa hawa walimu wapya nawashauri waende kuripoti katika vituo
walivyopangiwa na wakubali kufanya kazi katika maeneo hayo, sio waripoti
halafu waondoke,” alisema.
Wakati
huohuo, Serikali imewataka Makatibu Tawala wa Mikoa ambayo shule zake
zimefungwa kwa madai ya ukosefu wa chakula, kuwachukulia hatua wakuu wa
shule hizo, kwa kile kilichoelezwa kuwa wamekiuka utaratibu kutangaza
hivyo ilhali serikali ilishatuma fedha kwa ajili ya chakula cha
wanafunzi katika shule mbalimbali nchini.
Shule
zilizofungwa kwa tatizo hilo na mikoa yake kwenye mabano ni Rugambwa,
Kahororo, Nyakato na Ihungo (Kagera), Lyamungo (Kilimanjaro), Mpwapwa na
Abeid Karume (Dodoma), Kazima, Milambo, Wavulana Tabora na Wasichana
Tabora (Tabora).
Uamuzi
huo umetangazwa na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Jumanne Sagini aliyesema serikali
imeshatoa asilimia 66.7 ambazo ni Sh bilioni 28.1 zilizotengwa kwa mwaka
2014/2015.
Alisema
serikali imetoa fedha hizo katika kipindi cha mwezi Julai mwaka jana
hadi Machi mwaka huu kwa ajili ya chakula cha wanafunzi wa shule za
sekondari, zinazomilikiwa na serikali. Sagini alisema serikali ilitenga
Sh bilioni 42.1 kwa mwaka 2014/2015, ambapo kati ya fedha hizo kiasi
kilichobaki ni Sh bilioni 13.9, sawa na asilimia 33.23 ya fedha
zilizotengwa.
“Kwa
ufupi, serikali haijafunga shule na wakuu wa shule waliotangaza kufunga
shule hizo chache wamefanya makosa kwa kuwa hawakuwasiliana na mamlaka
husika ili kupata kibali kama kungekuwa na sababu ya kufanya hivyo,
naamini mamlaka husika zitawachukulia hatua,” alisema Sagini.
Alisema
wamiliki wa shule ni Mamlaka za Serikali za Mitaa, ambazo watendaji wake
ni wakurugenzi na wakuu wa shule ni viongozi wasimamizi wa shule hizo,
hivyo hawana mamlaka ya kutangaza kufunga shule kwa sababu yoyote bila
kibali cha mwenye shule.
Kwa
mujibu wa Sagini, kuna utaratibu wa kufunga shule ambapo katika kipindi
hiki, shule nyingi zilikuwa zimefungwa kwa mapumziko mafupi kati ya
Machi 28 hadi Aprili 12, ambapo katika shule hizo zilizofungwa wanafunzi
walilazimika kurudi makwao kutokana na kutangaziwa na wakuu wao wa
shule.CHANZO: HABARI LEO
No comments:
Post a Comment