Monday, April 20, 2015

Chadema: Zitto ni adui yetu namba moja

MNYIKA
Na Bakari Kimwanga, Mwanza

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetangaza kuwa adui yake namba moja ni Kiongozi Mkuu wa Chama cha Alliance for Change and Transparance (ACT-wazalendo), Zitto Kabwe.

Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Bara, John Mnyika akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Furahisha Mwanza juzi, alisema Chadema haiko tayari kuikaribisha ACT-Wazalendo ndani ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutokana na kile alichosema 'ni adui kwao'.
"Mtume Muhamad (S.A.W) alikuwa anazungumzia unafiki ambao una sura mbili na sifa zake, leo (ACT) wanasema wapo upinzani, wanasema msiunge mkono Ukawa halafu mnawakaribisha?

"Nendeni kila mahali waambieni wananchi adui yetu mkuu ni Zitto. Sikilizeni niwaambie Taifa hili kama ni ufisadi tumeshazungumzia sana kuanzia EPA mpaka Richmond. Dk. Slaa (Willbrod) alipoingia bungeni aliyasema haya kwa sasa si mapya. Adui yetu ni Zitto na hatumtaki Ukawa," alisema Mnyika.

Alisema Chadema haiko tayari kuikaribisha ACT-Wazalendo Ukawa kwa sababu adui kwao.
Zitto ajibu
Akihutubia mamia ya wananchi wa Mwanza jana, Zitto alisema kadri siku zinavyosonga wabaya wake wamekuwa wakijionyesha.
Zitto alisema pamoja na hali hiyo, ACT-Wazalendo haiko tayari kuzungumzia siasa za wakati uliopita kwa vile kufanya hivyo si afya njema kwa siasa za upinzani.
Alisema ni vema viongozi wa vyama vya upinzani waachane na ugomvi binafsi na watangulize masilahi ya taifa mbele.

"Mwanzo walipotufukuza walituambia tukatafute vyama vingine hilo likafanyika, tulipopata vyama vya kufanyia siasa wakasema vipo kwa ajili ya kugawa upinzani tukasema tupo tayari kuunganisha nguvu ya pamoja kwa ajili ya kuiondoa CCM...wenzetu pia hili hawalitaki sasa ni wajibu wenu kutambua watu gani hawataki kuiondoa CCM," alisema Zitto.
Alisema wao (ACT) wana nia ya dhati lakini wenzao wanaweka ugomvi binafsi mbele ya masilahi ya taifa.

"Sisi ACT Wazalendo bado tupo tayari kushirikiana kwa mujibu wa misingi. Shabaha yetu ni moja tu, kubomoa mfumo wa uchumi wa kinyonyaji na ufisadi ili kujenga uchumi shirikishi wa wananchi," alisema na kuongeza:
"Sikufundishwa kugombana na watu barabarani au kusema ovyo mitaani, kufanya hivi hakuna tofauti na kumsema mke au mume mlioachana...mmoja kwa kukosa busara na kwa kuwa aliachana na yule mke anaamua kwenda vijiweni na kutoa siri za mzazi mwenzie, hili kwetu hapana.
"Tunakuja na jahazi jipya ambalo ndugu zangu wa Mwanza nimekuja kuwakabidhi, kubwa tunataka kulirudisha taifa katika misingi yake ya ujamaa na kujitegemea, tunahitaji ujamaa wa demokrasia," alisema Zitto.

Alisema tafsiri ya ujamaa haina maana kuwa chama hicho kitataifisha mali za watu, bali kitarekebisha makosa ya ubinafsishaji kwa kurejesha mali zote za taifa zilizouzwa na wanunuzi hawajatekeleza mikataba yao.

Mapokezi Zitto ambaye amefuatana na Mwenyekiti wa chama hicho, Anna Mghwira, waliwasili Mwanza saa 8.00 mchana na kupata mapokezi makubwa yaliyoanzia wilayani Misungwi.
Mapokezi hayo yaliongozwa na vijana waendesha pikipiki (bodaboda) na kikundi cha wanawake ambao muda wote walikuwa katika shamrashara hadi alipoingia kwenye uwanja wa Furahisha.CHANZO:MTANZANIA(Muro)

No comments: