Friday, May 1, 2015

KIONGOZI WA WAASI WA ADF ATIWA MBARONI NCHINI TANZANIA


Kiongozi wa waasi wa ADF, Jamil Mukulu (menye shati jeupe).
Waasi wa Allied Democratic Forces  (ADF).
Raia wakikimbia mapigano dhidi ya ADF.
JEESHI  la polisi nchini limefanikiwa kumtia mbaroni kiongozi wa kundi la waasi wa Allied Democratic Forces  (ADF) wa nchini Uganda,  Jamil Mukulu,  ambaye amekamatiwa nchini Tanzania.
Mukulu  aliyekuwa akiongoza waasi hao katika mauaji wa halaiki katika nchi za Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) tangu miaka ya 1990, alikamatwa nchini Tanzania mwanzoni mwa mwezi huu akitokea mashariki mwa DRC.
Vyombo vya habari nchini Uganda vimethibitisha kutiwa mbaroni mtu huyo ambaye kundi lake linatuhumiwa kufanya mauaji ya watu 300 tangu mwezi Oktoba  mwaka jana hadi sasa huko DRC.
Mukulu ametiwa mbaroni kwa ushirikiano wa polisi wa Tanzania na wenzao wa Uganda. Hata hivyo,  jeshi la Uganda limesema kuwa haliwezi kuthibitisha kuwa mtu aliyetiwa mbaroni ni Jamil Mukulu hadi atakapofikishwa nchini humo na kuchukuliwa vipimo vya vinasaba vya DNA.
Kwa muda mrefu polisi ya Uganda ilikuwa imetoa amri ya kutiwa mbaroni kiongozi huyo wa waasi wa ADF mwenye umri wa miaka 51 kwa tuhuma za kufanya mauaji ya kigaidi na kuiomba Interpol iisaidie kumkamata.
Mukulu aliyekuwa muumin wa kanisa Katoliki kabla ya kuhamia Uislam, alianzisha kundi hilo la ADF mnamo miaka ya 1990, kwa ajili ya kupingana na serikali ya Uganda.
Tangu hapo amekuwa akiongoza waasi katika mapigano ambayo yamepoteza maisha ya maelfu ya raia wa Uganda na DRC. Mukulu anakabiliwa na makosa ya ugaidi na uhaini.
Taarifa ya Umoja wa Mataifa inasema mwaka 1998, waasi wa ADF walifanya mauaji ya kinyama ya wanafunzi 80 walipokivamia chuo kimoja magharibi mwa Uganda.
Mwezi Novemba mwaka jana waasi hao waliwaua watu zaidi ya 100 ikiwa ni mwendelezo wa mashambulizi ya kutisha  Mashariki mwa DRC.
CHANZO:  BBC SWAHILI

No comments: