Waziri
Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa akisalimiana na Kamishina Mkuu wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rished Bade na Naibu wake, Lusekelo
Mwaseba (wapili kulia ) baada ya kuwasili kwenye bandari ya Dar es
salaam kutaka maelezo kuhusu upotevu wa makontena 349 yenye kodi ya
serikali ya thamani ya shilingi bilioni 80, Novemba 27, 2015. (Picha na
Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri
Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa akimwonyesha orodha ya makontena 349
yenye kodi ya serikali ya thamani ya shilingi bilioni 80 yaliyotoka
kwenye bandari ya Dar es salaam bila kulipiwa kondi, Kamishina Mkuu wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania , Rished Bade wakati alipotaka maelezo kuhusu
upotevu wa makontena hayo, bandarini jijini Dar es slaam Novemba 27,
2015. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri
Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa akimkabidhi Kamishina Mkuu wa Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA), Rished Bade orodha ya makontena 349 yenye
kodi ya serikali ya thamani ya shilingi bilioni 800 yalitoka kwenye
bandari ya Dar es salaam bila kulipiwa kodi. Mheshimiwa Majaliwa
alikwenda kwenye bandari ya Dar es salaam Novemba 27, 2015 kutaka
maelezo kuhusu kupotea kwa makontena hayo. (Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu)
Waziri
Mkuu, Majliwa Kassim Majaliwa akizungumza kwenye bandari ya Dar es
salaam alikokwenda Novemba 27, 2015 kutaka maelezo ya makontena 349
yaliyotoka kwenye bandari ya Dar es salam bila kulipiwa kodi na
kuikosesha serikali shilingi billioni 80. (Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu)
…………………………………………………………………………
*Ni kwa upotevu wa makontena 349, yana thamani ya sh. bilioni 80/-
WAZIRI MKUU Majaliwa Kassim
Majaliwa amewasimamisha kazi maafisa watano na watumishi watatu wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutokana na upotevu wa makontena 349
yenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni 80/-.
Akizungumza na viongozi wa Mamlaka
ya Bandari pamoja na viongozi wa TRA katika ziara ya kushtukiza leo
mchana (Ijumaa, Novemba 27, 2015), Waziri Mkuu amewataka Kamishna Mkuu
wa TRA, Bw. Rished Bade na Naibu Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Lusekelo
Mwaseba wahahakikishe wanashirikiana na polisi kufuatilia upotevu huo na
kwamba fedha hizo zinapatikana na zinarudi Serikalini.
Akitangaza uamuzi huo baada ya
kufanya kikao na baadhi ya viongozi wa Serikali bandarini hapo, Waziri
Mkuu aliwataja maafisa waliosimamishwa kazi kuwa ni Kamishna wa Forodha,
Bw. Tiagi Masamaki na Mkuu wa Kituo cha Huduma kwa Wateja, Bw. Habibu
Mponezya.
“Hawa wanasimamishwa kazi. IGP
ninaagiza hawa watu wakamatwe na kuisaidia polisi. Hati zao za kusafiria
zikamatwe na mali zao zikaguliwe kama zinaendana na utumishi wa umma,”
alisema Waziri Mkuu.
Maafisa wengine waliosimamishwa
kazi ni Mkuu wa kitengo cha TEHAMA, Bw. Haruni Mpande, Bw. Hamisi Ali
Omari (hakutaja ni wa idara gani), na Mkuu wa Kitengo cha Bandari Kavu
(ICD In-Charge), Bw. Eliachi Mrema. “Hawa wanasimamishwa kazi hadi
uchunguzi utakapokamilika na pia wawe mikononi mwa polisi,” alisema.
Pia aliagiza watumishi watatu wa
mamlaka hiyo wahamishwe kutoka Dar es Salaam na kupelekwa mikoani.
Watumishi hao ni Bw. Anangisye Mtafya, Bw. Nsajigwa Mwandengele na Bw.
Robert Nyoni.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu
amemwagiza Katibu Mkuu wa Hazina, Dk. Servacius Likwelile ambaye
alikuwepo kwenye kikao hicho, kuhakikisha kuwa anapeleka wataalamu
kutoka Wakala wa Serikali Mtandao (e-Govt) haraka iwezekanavyo ili
wakakague mifumo ya taarifa na kubaini jinsi ambavyo wizi huo
unafanyika.
“Ninataka uchunguzi uanze
kufanyika mara moja, tafuteni njia ambazo zinatumika kama mianya ya wizi
kutokea hapa bandarini hadi kwenye ICDs. Nataka hayo makontena
yatafutwe hadi yajulikane yako wapi, na fedha hiyo ihakikishwe inarudi
serikalini,” alisema.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Bw. Ernest Mangu, Katibu Mkuu wa Ofisi
ya Waziri Mkuu, Dkt. Florens Turuka, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi,
Dkt. Shaaban Mwinjaka, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya DSM, Suleiman
Kova, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari (TPA), Bw. Awadh Massawe na
viongozi mbalimbali kutoka TRA na TPA.
Mapema akijibu maswali ya Waziri
Mkuu, Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Bade alikiri kwamba kuna upotevu wa
makontena ambao huwa unafanyika kati ya bandarini na ICDs na hasa ICD ya
Ubungo. Akitoa ufafanuzi, alisema kwamba walifanya ukaguzi kwenye ICD
moja na kukuta makontena 54 yamepotea kwa njia za wizi. “Hata hivyo,
tulipoendelea na ukaguzi, namba iliongezeka na kufikia 327. Tunaendelea
kufuatilia kwa kushirikiana na TAKUKURU. Mmiliki wa ICD ametakiwa kulipa
faini sh. bilioni 12.6/- na ameshalipa sh. bilioni 2.4/-,” alifafanua.
Alipoulizwa na Waziri Mkuu kama
ana majina ya watumishi wanaohusika na wizi huo, Bw. Bade akakiri kwamba
anayo lakini siyo kwa wakati huo labda ayapate kutoka kwa wasaidizi
wake. Ndipo Waziri Mkuu akamuonyesha orodha ya makontena 349 yenye
taarifa zote hadi namba za magari yaliyobeba mizigo hiyo na Bw. Bade
akakiri kwamba orodha hiyo ni ya kweli.
“Kwa utaratibu huo hatuwezi
kufika, labda baadhi ya watu waondolewe kazini”. Ndipo akaanza kutaja
majina ya maafisa hao waliosimamishwa kazi.
No comments:
Post a Comment