Thursday, April 27, 2017

Babu Seya kuachiwa Huru


Tumaini jipya! Mtoto wa kiume wa mfungwa anayetumikia kifungo cha maisha jela, Nguza Viking ‘Babu Seya’, Mbangu Nguza ameibuka na kusema kuwa, mwaka 2017 ndiyo wa mwisho kwa baba yake na mdogo wake, Johnson Nguza ‘Papii Kocha’ kuendelea kutumikia kifungo chao cha maisha jela.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Gazeti Amani mwanzoni mwa wiki hii, Mbangu alisema kuwa, turufu ya mwisho ya hukumu ya ndugu hao ipo kwenye mikono ya Mahakama ya Haki za Binadamu Afrika (AfCPHR) yenye makazi yake jijini Arusha ambayo kimsingi vikao vitatu vya awali vimeshakaa na kubaini kuwa, hukumu ya Babu Seya na Papii ilikuwa na kasoro.

“Unajua watu hawafahamu, kule ambako hukumu ya mzee na bwana mdogo (Papii), ilipelekwa kuna hatua. Kwanza kabisa, wale majaji wanatoka nchi mbalimbali, kwa hiyo siyo kwamba wanakwenda tu Arusha na kupitia hukumu, hapana.

“Kilichofanyika ni kwamba, kuna watu walikaa mara tatu kupitia hukumu ili wajiridhishe kama kuna makosa ambayo majaji wakikaa watayaona?

“Kwa hiyo vile vikao vimeshakaa mara tatu zote na kubaini kuwa, kweli hukumu ya baba na bwana mdogo ilikuwa ina kasoro.

“Sasa ndiyo majaji wameitwa ili kupitia na kutoa hukumu yao ya haki. Hii kazi ingekuwa imeshafanyika muda mrefu ila sasa, kilichotokea ni kwamba, kuanzia Novemba mwaka jana kama sikosei, watu wa mahakamani walikuwa likizo ndefu mpaka kwenye Februari mwaka huu, ndiyo wamerudi.

“Kingine kimechelewesha ni mwaka jana kustaafu kwa rais wa ile mahakama, Jaji Augustino Ramadhani (kutoka Tanzania), kukawa na kitambo cha kusubiri kumpata rais mpya, tayari yupo (Sylvain Ore kutoka Cote d’Ivoire).

“Kwa hiyo bwana, baada ya sasa, wakati wowote ule, majaji watatua Arusha na kukaa kupitia, naamini, tena narudia kusema, naamini, baba na bwana mdogo wangu mwaka huu watakuwa huru.

“Hili suala la wao kuwa huru liko pia kiroho, hata kama mahakama hiyo isingekaa, bado wale ndugu wangetoka tu, lazima. Kwani Mungu ninayemtegemea mimi ameshaniambia watatoka,” alisema Mbangu ambaye kwa sasa ni Mwinjilisti wa Neno la Mungu.

No comments: