Wednesday, May 24, 2017

Majaliwa ataka benki kukopesha wakulima

BENKI za wakulima na taasisi za kifedha nchini zimetakiwa kuwakopesha wakulima ili wanunue zana za kilimo kwa lengo la kuboresha kilimo ili kiwe na tija.

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipotembelea kampuni ya kuunganisha matrekta ya Ursus kutoka Ujerumani, ambako pia alitembelea Kituo cha Uwekezaji cha EPZA na kiwanda cha ulainishaji vyuma cha Kamal Industrial Estate kilichopo wilayani Bagamoyo wakati wa ziara yake mkoani Pwani ya kutembelea viwanda.

Waziri Mkuu alisema ili dhana ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na uchumi wa kati lazima vyanzo vya kuinua uchumi viwekewe mazingira mazuri. “Tumeshazungumza na mabenki ya kilimo na taasisi za kifedha ili ziwakopeshe wakulima waweze kununua zana za kilimo kwa mkopo na walipe kwa awamu,” alisema Majaliwa, na kuongeza kuwa serikali ina mpango wa kuwa na viwanda vingi ili kuinua kipato cha Watanzania na kuwa na uchumi wa kati kwa kuwawekea mazingira ya kiuchumi.

“Kuanzishwa kwa viwanda hivi kumefungua fursa kwa wajasiriamali wadogo kwa kufanya biashara ndogondogo ikiwa ni pamoja na uuzaji wa vyakula, vinywaji na vitu vingine,” aliongeza.

Aidha, alisema serikali imeweka mazingira mazuri kwa wawekezaji wa ndani na nje na kuwataka Watanzania wenye marafiki wa nje wenye uwezo wa kuanzisha viwanda wawaite ili wawekeze.

Naye Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alisema mradi huo ni endelevu wa kuunganisha matreka kwa lengo la kuboresha kilimo ili kiwe na tija na kuinua uchumi wa wananchi.

Mwijage alisema hadi sasa kiwanda hicho tayari kimeunganisha matrekta 2,400 ambayo yatasambazwa nchi nzima ambapo kutaanzishwa vituo vinane kwa ajili ya kuwafikia wananchi.

“Uanzishwaji wa kiwanda hicho kumeleta manufaa kwani tayari vijana wamepata kazi moja kwa moja toka vyuoni kama ilivyokuwa zamani na hii ndiyo faida ya uanzishwaji wa viwanda,” alisema.

Alisema kwa sasa TRA wamewapa msamaha wa kodi kiwanda hicho hivyo kusaidia matreka mengi kuingia kwa urahisi ambapo zamani kulikuwa na gharama kubwa sana za ushuru.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo alisema kwa sasa Mkoa wa Pwani umefanikiwa kuwa na viwanda vikubwa 84 kati ya viwanda 393 nchini; na kwamba tatizo ni upungufu wa umeme wa uhakika ambapo mkoa unahitaji megawati 60 ambapo kwa sasa mkoa unapata megawati 48.
Post a Comment