Sunday, May 28, 2017

Rais Magufuli atembelea Muhimbili

 Rais John Magufuli leo amewajulia hali wagonjwa waliolazwa katika wodi ya Mwaisela iliyopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na kuwashukuru madaktari na wauguzi kwa juhudi kubwa wanazofanya kunusuru maisha ya watu.

Rais Magufuli akiwa na mkewe Mama Janeth Magufuli wamewatembelea wagonjwa hao majira ya saa moja ya asubuhi wakitokea katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Petro lililopo Oysterbay jijini Dar es Salaam ambako wamehudhuria ibada ya Jumapili.

Miongoni mwa wagonjwa waliojuliwa hali na Rais Magufuli na mkewe ni Mzee Francis Maige Kanyasu (Ngosha) aliyelazwa katika chumba namba 310 na Mtoto Shukuru Musa Kisonga aliyelazwa katika chumba namba 312 ambaye hivi karibuni aliripotiwa kuugua ugonjwa usiofahamika uliosababisha aishi kwa kunywa mafuta ya kula, sukari na maziwa.

Pamoja na kuwapa pole wagonjwa waliolazwa katika wodi ya mwaisela na kuwashukuru madaktari na wauguzi, Rais Magufuli amesema Serikali itaendelea kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili hospitali hiyo na changamoto zinazowakabili madaktari na wauguzi.

“Jamani, madaktari tunawashukuru sana, mnafanya kazi nzuri, Madaktari wote nchini pokeeni pongezi zangu, sisi Serikali tutaendelea kuzikabili changamoto hizo na siku moja zitakwisha, kikubwa ni kumtanguliza Mungu mnapofanya kazi ya kuokoa maisha ya watu kwa juhudi kubwa, mnafanya kazi ya Mungu” amesema Rais Magufuli.
Post a Comment