Wednesday, May 31, 2017

SIMANZI KWA TAIFA...

Rais Magufuli amlilia Mwasisi wa Chadema

Rais John Magufuli amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha  mmoja wa waasisi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, (Chadema) Phillemon Ndesamburo huku akimtaja marehemu kuwa alikuwa kiongozi mwenye hekima na aliyezingatia siasa za kistaarabu.

Taarifa iliyotumwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa  leo Jumatano imeeleza kuwa Rais Magufuli , ametuma salamu za rambirambi kwa viongozi na wanachama  wa Chadema pamoja na ndugu, jamaa na marafiki wote walioguswa na kifo hicho.

“Kwa masikitiko nimepokea taarifa za kifo cha Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Moshi Mjini, Mzee wangu Philemon Ndesamburo. Namkumbuka Mzee Ndesamburo kwa hekima zake na uongozi wake uliozingatia siasa za kistaarabu,”imesema taarifa hiyo

Rais Magufuli amesema alifanya kazi na Ndesamburo wakati wote wakiwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wakati wote walishirikiana, kutaniana na anamkumbuka kwa namna ambavyo alitumia muda wake bungeni kupigania mambo yenye maslahi kwa wananchi wa jimbo lake la Moshi Mjini.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Magufuli ameitaka familia ya Ndesamburo na wote walioguswa na msiba huu kuwa na moyo wa subira na uvumilivu
.................................................................................................................................

Ndugai amkumbuka Ndesamburo kipekee


Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema anamkumbuka marehemu Phillemon  Ndesamburo aliyekuwa mbunge wa Moshi  Mjini (Chadema) kwa uchapakazi wake na mapenzi yake makubwa kwa wapiga kura wake.

“Nimepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Mheshimiwa Ndesamburo ambaye pia ni baba wa Mbunge wa Viti Maalum,  Lucy Owenya kilichotokea leo Mkoani Kilimanjaro, hakika ni pigo kubwa,”amesema Spika katika taarifa iliyotumwa leo  na Kitengo cha Mawasiliano cha ofisi yake

Ndesamburo amefariki leo wakati akipata matibabu katika hospitali ya Rufaa ya KCMC.

Taarifa hiyo imeongeza; "Namkumbuka vyema marehemu Ndesamburo na tuliingia Bungeni pamoja mwaka 2000, alikuwa na mapenzi makubwa kwa wapiga Kura wake."

............................................................................

Alichosema Lowassa baada ya Kifo cha Ndesambulo

Mjumbe wa Kamati ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa ameeleza kusikitishwa na kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo (Chadema) na kueleza kuwa alikua shujaa wa mabadiliko.

Lowassa kupitia ukurasa wake wa mtandao wa twitter ametweet, “Nimesikitishwa sana na kifo cha ghafla cha Mzee Ndesamburo, Mungu ailaze roho yake mahala pema peponi natoa pole kwa familia na wote. Mzee Ndesamburo alikua shujaa wa kweli wa mabadiliko wa miaka mingi na mwenye mchango mkubwa kwenye siasa za demokrasia katika Taifa letu

Ndesamburo aliyekuwa Mbunge kuanzia mwaka 2000 hadi 2015 amefariki dunia ghafla leo hii wakati akipata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Moshi mkoani Kilimanjaro.

............................................................................

Zitto : Huwezi kutaja maendeleo ya Chadema bila ya kumta Mzee Ndesemburo


Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo) Zitto Kabwe ametuma salamu za rambi rambi kwa wanachama wa Chadema  baada ya kuondokewa na kiongozi wake mkubwa, Philemon Ndesamburo.

 Pia Zitto amempa pole, mtoto wa marehemu Ndesamburo, Lucy Owenya kwa kumpoteza baba yake.

 “Huwezi kutaja maendeleo ya Chadema kwa nchi yetu bila ya kutaja jina la mzee Ndesamburo. Nimepata bahati ya kufanya naye kazi kwa karibu, naweza kutamka bila wasiwasi kwamba ni mmoja wa watu waliokipenda chama chake kwa dhati kabisa,” amesema


Zitto ameandika katika ukurasa wake wa Facebook leo na kusema; “Ni msiba mkubwa kwa watu wa Kilimanjaro na hasa Moshi Mjini ambapo Mzee Ndesa Pesa alikuwa mwakilishi wake Bungeni kuanzia Mwaka 2000 mpaka Mwaka 2015. Kilimanjaro imepoteza mtu ambaye aliweka maslahi ya mkoa wake mbele kuliko kitu kingine chochote.”

Zitto amesema msiba wa Ndesamburo ni mkubwa kwa wanaChadema ambacho alikuwa Mwenyekiti wake wa  Mkoa tangu chama kimeanzishwa mpaka mauti yalipomkuta.

Kadhalika Zitto anaendelea kummwagia sifa Ndesamburo akisema Tanzania ina faidi matunda ya vyama vingi kwa sababu ya kazi kubwa aliyofanya Mzee Ndesamburo.

“Nawapa pole Sana watoto, wajukuu na vitukuu vya Mzee Ndesamburo. Mzee wetu aliishi maisha yake na ameacha ' legacy ' yake. Najua maumivu yenu lakini tupo wengi tunaoumia nanyi. Mungu awavushe kwenye mtihani huu mkubwa. muwe wamoja na mshikamane.” Amesema na kuongeza:

“Poleni sana ndugu zangu wa Chadema kwa kupotelewa na kiongozi wenu na kiongozi wetu pia.  Poleni sana wana Moshi Mjini na wana Kilimanjaro wote. Poleni Sana Watanzania.pumzika kwa Amani Philemon Kiwelu Ndesamburo. Hiyo ni njia yetu sote. Amina.”
....................................................................................................................................

Ndugu wataka uchunguzi kifo cha Ndesambulo

Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Kilimanjaro, Mzee Philemone Ndesamburo amefariki Dunia asubuhi ya leo katika Hospitali ya KCMC, Mkoani humo.

Katibu wa Chadema mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema amethibitisha muda huu juu ya kifo hicho na kwamba bado haijafahamika chanzo cha kifo chake.

Kwa sasa mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti hospitali ya rufaa ya KCMC.

Ndugu wakiwemo watoto wa marehemu wamefika Hospitalini hapo na kuomba mwili wa marehemu kufanyiwa uchunguzi kutokana na kifo kuwa ni cha ghafla.

Lema alisema, Mzee Ndesamburo alifika ofisini kwake majira ya asubuhi na alionekana mwenye afya njema, ilipofika majira ya saa nne hali ilibadilika na kushindwa kuendelea na majukumu yake.

Ndipo walipomkimbiza KCMC kwa ajili ya matibabu na alifariki dunia akiwa kitengo cha wagonjwa mahututi, Taarifa zaidi tutajulishana kadri zitakapokuwa zikitufikia.
BWANA ALITOA NA BWANA AMETWAA JINA LA BWANA NA LIHIMIDIWE

Post a Comment