Saturday, May 27, 2017

Tanzania ,Uganda wasaini Dili hili la Mradi wa Bomba la Mafuta


SERIKALI ya Tanzania na Uganda zimetiliana saini Mkataba wa Ujenzi wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga nchini Tanzania lenye urefu wa Kilometa 1,443, uliokadiriwa kugharimu zaidi ya Dola bilioni 3 nukta 55, mjini Kampala Uganda, leo.

Mkataba huo umesainiwa na Waziri wa Katiba na Sheria wa Tanzania, Profesa Paramagamba Kabudi na Waziri wa Nishati wa Uganda, Mhandisi Irene Muloni.

Tukio hilo limefanyika siku chache baada ya marais wa nchi hizo mbili, John Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Uganda, Yoweri Museveni, kutia saini tamko la pamoja la kukamilika kwa majadiliano ya vipengele vya mkataba, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Hafla ya kutia saini mkataba huo iliyofanyika katika Hoteli ya Serena, Jijini Kampala, Uganda imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa nchi zote mbili wakiwamo mawaziri, makatibu wakuu, wanasheria wakuu wa Serikali, wakurugenzi na viongozi wa taasisi mbalimbali zinazohusika katika mradi huo.

Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima-Uganda hadi Tanga Tanzania, unatarajia kusisimua uchumi wa nchi hizo mbili na katika mchakato wa ujenzi wake zaidi ya watu 10,000 wanatarajiwa kunufaika na ajira.

Hivi Karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Magufuli aliuelezea mradi huo kuwa ni mkubwa kwakuwa Uganda imegundua shehena kubwa ya mafuta katika eneo la Hoima kiasi cha mapipa bilioni 6 na laki 5 na kwamba Tanzania inatarajia pia kupata mafuta kule ziwa Tanganyika na ziwa Eyasi, ambayo yatapitishwa katika bomba  hilo hilo.
Post a Comment