Monday, May 22, 2017

Trump apania kusuluhisha mgogoro wa Israel na Palestina


Rais wa Marekani baada ya kumaliza ziara yake suadi arabia leo ameanza ziara yake ukanda wa nchi za Mashariki ya kati ambapo ameanza taratibu za kuketi pamoja na viongozi wa nchi ya Israel na Palestina

Bw Trump anatarajiwa kufanya mazungumzo na viongozi wa Israel na Palestina katika kipindi cha siku mbili atakazokuwa eneo hilo.

Rais huyo amesema kupatikana kwa mkataba wa amani kati ya Waisraeli na Wapalestina yatakuwa mafanikio makubwa, lakini hakusema mkataba kama huo unafaa kuchukua mwelekeo gani.
Amesema angependa sana pande zote mbili ziamue kuhusu mkataba huo wa amana kwa mashauriano ya moja kwa moja.

Katika mkutano mkuu wa viongozi wa Kiislamu na Kiarabu mjini Rihadh siku ya Jumapili, Bw Trump aliwataka viongozi hao kuwa kwenye mstari wa mbele katika kukabiliana na wanamgambo wa Kiislamu na wapiganaji wenye itikadi kali na "kuwafurusha kutoka kwenye dunia hii."

Aliitaja moja kwa moja Iran na kusema kwamba imekuwa "ikichochea mizozo ya kidini na ugaidi" katika kanda hiyo kwa miongo mingi.

Bw Trump pia alikariri tena kwamba anaamini amani kati ya Waisraeli na Wapalestina inaweza kupatikana.

Rais huyo wa Marekani amekuwa akichukuliwa sana kuwa muungaji mkono mkubwa wa Israel kuliko mtangulizi wake Barack Obama.

Amechukua msimamo usio mkali kuhusu suala tata la Israel kujenga makazi ya walowezi maeneo ya Wapalestina na kudokeza kwamba upanuzi wa makao hayo na si kuwepo kwa makao yenyewe, unaweza kuwa ndio kikwazo katika kutafuta amani.

Zaidi ya Wayahudi 600,000 huishi katika makao makazi 140 ya walowezi ambayo yamejengwa tangu Israel ilipotwaa maeneo ya Ukingo wa Magharibi na Mashariki mwa Jerusalem mwaka 1967, maeneo ambayo Wapalestina huyachukuliwa kuwa sehemu ya "taifa litakaloundwa" la Wapalestina.
Makazi hayo ni haramu chini ya sheria za kimataifa, lakini Israel hupinga hilo.

Rais huyo pia ametoa ishara za kukanganya kuhusu mji wa Jerusalem, na kuahidi kuhamishia ubalozi wa Israel mjini humo kutoka Tel Aviv, hatua iliyowakera Wapalestina lakini ikawafurahisha sana Waisraeli.

Hata hivyo, baadaye alionekana kulegeza msimamo huo, na Waziri wa Mambo ya Nje Rex Tillerson majuzi aliambia NBC News kwamba Bw Trump bado analitafakari jambo hilo.

No comments: