Friday, June 2, 2017

Idadi ya watu wanaosafiri kwenye mabasi ya mwendokasi kila siku

Dar es Salaam. Mradi wa mabasi yaendayo haraka (BRT) sasa unasafirisha watu 200,000 kwa siku kutoka watu 50,000 iliyokuwa ikisafirisha mwaka jana baada ya mradi huo kuanza kazi.

Kuongezeka kwa idadi hiyo inaelezwa kuwa ni ishara ya wananchi kuukubali mradi huo na kuutumia kila siku waendapo sehemu zao za kazi au majumbani.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika waliotembelea mradi wa BRT, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usafiri wa Haraka Dar es Salaam (DART), Hazina Mfinanga amesema mafanikio ya mradi huo yametokana na ushirikiano mkubwa uliopo baina ya wadau mbalimbali.

Mfinanga amewataja wadau hao kuwa ni kampuni ya UdaRT ambayo ndiyo inaendesha mabasi, Maxcom Africa ambao wanaendesha mifumo ya kukusanya nauli na benki ya NMB ambayo inasimamia upatikanaji wa fedha za mradi huo.

"Bado tuko kwenye kipindi cha majaribio wakati tukiendelea na mchakato wa kupanua njia za BRT katika jiji hili ili watu wengi zaidi waweze kunufaika na mradi huu," amesema Mfinanga.

Mfinanga ambaye pia ni Meneja Rasilimali watu wa DART, amesema wazo la kuanzisha mradi huo lilikuwa ni kutatua changamoto zinazowakabili wakazi wa Dar es Salaam ambazo ni pamoja na kupoteza muda kwenye foleni na uchafuzi wa mazingira.
Post a Comment