Tuesday, June 6, 2017

Mdee, Bulaya kulipwa nusu mshahara kwa miezi 10 nje ya Bunge

Dodoma. Wabunge wa Chadema, Halima Mdee (Kawe) na Ester Bulaya (Bunda Mjini) ambao wamesimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge, watalipwa nusu mshahara na posho zinazoambatana nao kwa miezi kumi.

Stahiki hizo ni kwa mujibu wa kanuni ya 75 ya Bunge inayosema, “mbunge aliyesimamishwa hataingia tena sehemu yoyote ya ukumbi na maeneo ya Bunge kwa muda wote atakapokuwa amesimamishwa na atalipwa nusu mshahara na nusu posho zinazoambatana na mshahara huo.”

Vilevile, kutokana na uamuzi huo wabunge hao watakosa siku 65 za Bunge zinazojumuisha siku 25 zilizobaki za Bunge la bajeti linaloendelea, Bunge la Oktoba na lile la Februari, 2018. Vikao vya mabunge hayo mawili; la Oktoba na Februari kila kimoja huwa na mikutano ya wiki mbili mbili.

Wabunge hao walisimamishwa jana kwa azimio la Bunge licha ya kutokuwapo au kujitetea kutokana na tuhuma zilizokuwa zinawakabili za kudharau kiti cha spika.

“Tukutane Bunge lijalo la bajeti,” alisema jana Spika wa Bunge, Job Ndugai. Bunge la bajeti huanza mwezi Aprili.

Kufikia uamuzi huo, kamati ya haki, maadili na madaraka ya Bunge ilisema iliwatafuta kwa simu wabunge hao, lakini haikuwapata. Pia, iliwatumia ujumbe mfupi ambao haukujibiwa na ilipowapelekea hati ya wito haikuwakuta majumbani kwao.

Kwa kutambua umuhimu wa agizo ililonalo na kuzingatia matakwa ya kisheria, hati hizo ziliachwa baada ya kuelezwa kwamba wahusika hawapo kwani wamesafiri. Baada ya jitihada hizo kushindwa kuzaa matunda, kamati iliendelea kuwajadili bila wao kuwapo na kutoa maazimio hayo.

Maazimio yalivyo

Baada ya uchunguzi wa tuhuma za wahusika, kamati ilipendekeza Bulaya na Mdee wasihudhurie vikao vyote vilivyobaki vya mkutano wa saba wa Bunge la bajeti kuanzia tarehe ya azimio hilo na vikao vyote vya mkutano wa nane isipokuwa siku ya mwisho ya mkutano huo.

Mbunge wa viti maalumu (CCM), Juliana Shonza aliliongezea makali zaidi azimio la kamati hiyo kwa kupendekeza kuwa wabunge hao wasihudhurie vikao vyote vilivyobaki vya mkutano wa saba wa Bunge la Bajeti, mkutano wote wa nane na mkutano wote wa tisa.

Ilipendekezwa na kamati, kwamba Bulaya na Mdee wasihudhurie vikao vyote vilivyobaki vya mkutano wa saba na vikao vyote vya mkutano wa nane isipokuwa siku ya mwisho.

Lakini Shonza alitaka wabunge hao kutohudhuria vikao vyote vilivyobaki vya mkutano wa saba, wa nane na tisa na kufanikiwa kuwashawishi wabunge wengi waliokubaliana naye.

Kwa kauli ya wengi, wabunge hao wawili wamefungiwa. Akihitimisha hukumu hiyo, Spika Ndugai alisema wabunge hao watakosa vikao vilivyobaki vya Bunge linaloendelea, mkutano mzima wa Oktoba na hata ule wa Februari mwakani.

“Hawa tutakutana kwenye Bunge la bajeti linalokuja. Anayetaka kwenda popote pale na aende. Na maamuzi yoyote yale yanayofanywa, itakuwa ndio mwanzo wa constitution crisis (mgogoro wa kikatiba) katika nchi hii kama mimi ndiye spika,” alisema Ndugai.

Kwa kusisitiza kilichoafikiwa na Bunge, spika alisema endapo yeyote atachukua hatua za kupinga hilo, “tutarudi tena hapa na badala ya adhabu ya mwaka mmoja tutapiga miaka kadhaa halafu tuone kitakachotokea. Hatuwezi kuona Bunge hili linavurugwa. Hatuwezi.”

Hoja za msingi

Kamati ilimchunguza Bulaya na kujiridhisha kwamba ni kweli alidharau mamlaka ya spika kwa kukaidi maelekezo yake ya kumtaka atulie ili kumruhusu Livingstone Lusinde aliyekuwa amepewa nafasi ya kuzungumza aendelee kuchangia mjadala wa Wizara ya Nishati na Madini.

Vilevile, ilijiridhisha kwamba Bulaya alidharau mamlaka ya spika kwa kuwahamasisha wabunge wa kambi rasmi ya upinzani kutoka nje wakati kikao kikiendelea.

Tuhuma yake ya tatu ilikuwa kusimama na kusema bungeni bila kufuata taratibu na kanuni zinazoliongoza Bunge hilo.

Kwa upande wa Mdee, kamati ilijiridhisha kwamba alidharau mamlaka ya spika kwa kuwafanyia fujo askari waliokuwa wameamriwa kumtoa nje Mbunge wa Kibamba (Chadema), John Mnyika ambaye kiti kilidai alionyesha utovu wa nidhamu kwa kubishana nacho akitaka aliyemuita mwizi awajibishwe.

Kwenye tuhuma zote, wabunge hao walikutwa na hatia hivyo, kuishawishi kamati kupendekeza adhabu ambazo zilipaswa kuridhiwa na Bunge.

Akitoa maoni, Mwenyekiti wa kamati, George Mkuchika alisema, “ilijiridhisha bila kuacha shaka yoyote kuwa watuhumiwa walidharau mamlaka ya spika kinyume na kanuni za Bunge.”

No comments: