Wednesday, June 14, 2017

Wabunge watakiwa kuweka uzalendo mbele

Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga kimewataka wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kutanguliza uzalendo wakati watakapofanya marekebisho ya sheria za madini ili kunusuru raslimali za nchi  zisiendelee kuporwa.

Wito huo ulitolewa leo Jumatano na Katibu wa CCM Mkoa wa Tanga, Allan Kingazi wakati akitoa tamko la kumuunga mkono Rais John Magufuli katika kupambana na uporaji wa mchanga wa madini na rasilimali za madini kwa ujumla.

Akizungumza mbele ya  wajumbe wa NEC, wajumbe wa kamati ya siasa, jumuiya za chama hicho, viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini na wawakilishi wa makundi ya kijamii, Kingazi amesema wabunge wana nafasi kubwa ya kurekebisha sheria ya madini ikawa na manufaa, iwapo wataweka mbele maslahi ya nchi.

Alisema katika kupigania rasilimali za nchi hakuna sababu kwa wabunge kugawanyika kwani watatoa mwanya kwa wasioitakia mema Tanzania kuendeleza uporaji wa mali za nchi.

“CCM Tanga tunamuunga mkono Rais John Magufuli, rasilimali za madini zinazoporwa, ameamua kuweka uzalendo mbele na kupambana na waporaji ambao wamekuwa wakifaidika huku nchi ikididimia kiuchumi,”amesema Kingazi.

Akizungumza kwa niaba ya wazee wa Tanga, Abdallah Mnyamisi (81) alisema kinachofanywa na Rais Magufuli kinawakumbusha enzi zao ambapo kuanzia Mwalimu Nyerere hadi viongozi wengine hawakukubali  kununuliwa na matajiri  na ndiyo maana hadi sasa nchi ya Tanzania ina rasilimali za kutosha.

“Tunakupongeza Rais Magufuli, unaandika historia isiyofutika kwa hili nafahamu utakuja kukumbukwa na vizazi vijavyo, endelea sisi wazee tunakuunga mkono,”amesema Mnyamisi.

Mwenyekiti wa  umoja wa makanisa mkoa wa Tanga, Askofu Jothan Mwakimage, alisema viongozi wa dini wanaunga mkono harakati za Rais Magufuli za kupigania haki za wanyonge  ikiwamo kufichua wizi katika madini na kumtaka kutoogopa kwa sababu kila siku wamekuwa wakimuombea kwa Mungu.

No comments: