Monday, July 17, 2017

Kilichomuua Mke wa Mwakyembe

Linah ambaye alikuwa amelazwa akitibiwa katika Hospitali ya Aga Khan ya jijini Dar es Salam kwa muda mrefu, anatarajiwa kuzikwa keshokutwa wilayani Kyela mkoa wa Mbeya, familia ilisema zaidi jana.

Linah ameacha mume na watoto watatu.

Msemaji wa familia ya Waziri Mwakyembe, Solomon Kivuyo ndiye aliyetoa tarifa hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari waliofika nyumbani kwa marehemu, Kunduchi Beach, Manispaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

"Alikuwa akisumbuliwa na saratani ya titi kwa zaidi ya miaka miwili na alishawahi kutibiwa hospitali za hapa nchini, India na hata Uturuki," alisema Kivuyo ambaye alijitambulisha zaidi kuwa shemeji wa marehemu.

Kivuyo ambaye ni mtumishi ofisi ya Rais-Ikulu alisema baadhi ya ndugu wa familia wataanza safari ya kuelekea Mbeya kwa ajili ya mazishi leo, huku wengine wakitarajiwa kuondoka kesho.

Wakati huohuo, Rais John Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa Waziri Mwakyembe kufuatia kifo cha mkewe.

Taarifa iliyotumwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa ilieleza Dk. Magufuli ameshtushwa na kusitishwa na kifo hicho na kusema familia yake inaungana na familia ya Dk. Mwakyembe katika kipindi hiki kigumu.

"Nakupa pole sana Dk. Mwakyembe kwa kuondokewa na mkeo mpendwa Bi. Linah," taarifa ya Ikulu ilimkariri Rais Magufuli akisema na kueleza zaidi:

"Natambua hisia za maumivu ulizonazo wewe na familia nzima, nyote nawaombea mwenyezi Mungu awatie nguvu, awape subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.

"Namuombea marehemu apumzike mahali pema peponi."

Aidha, viongozi mbalimbali wa serikali na wabunge walifika nyumbani kwa Waziri Mwakyembe kumpa pole wakiwamo Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Elisante Ole Gabriel na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Modestus Kipilimba.

Akizungumza katika msiba huo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema kesho Makamu wa Rais Samia Suluhu atahudhuria shughuli za kuaga mwili wa marehemu.

Alisema yeye (Waziri Mkuu) ataiwakilisha serikali katika mazishi yatakayofanyika wilayani Kyela mkoani Mbeya, na kwamba Serikali itatoa ndege kwa ajili ya kuusafirisha mwili wa marehemu.
Post a Comment