Tuesday, July 4, 2017

Rais Magufuli apiga marufuku utoaji wa leseni za kuchimba madini

Sengerema. 
Rais John Magufuli ameiagiza Wizara ya Nishati na Madini kusitisha utoaji wa leseni za uchimbaji wa madini kwa mwekezaji yeyote hadi serikali itakapojipanga upya.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo Jumanne Julai 4, wakati aliposimama kuzungumza na wananchi mjini Geita akiwa njiani kuelekea Chato akitokea Sengerema.

Rais amekwenda Chato kwa ajili ya mapumziko mafupi.

Amesema dhahabu iliyopo nchini ni kwa ajili ya wananchi wote hivyo mwekezaji anayetaka kuwekeza lazima akubali kuingia ubia na nchi na mikataba isainiwe hadharani bila kificho.

Amesisitiza kuwa serikali yake imedhamiria kuhakikisha kuwa rasimali za nchi zinawanufaisha wananchi wote na si wawekezaji wachache matapeli.

"Dhahabu ni yetu… lazima tuingie ubia tujue asilimia zetu na zake, sitaki wanaokuja kwa mwavuli wa mwekezaji na kututapeli… nasema tena fisadi ni fisadi awe mzungu au mwafrika," amesisitiza Rais Magufuli

Amebainisha kuwa anawapenda wawekezaji lakini hayupo tayari kuwakumbatia wawekezaji wanaonyonya rasilimali za nchi.

No comments: