Wednesday, July 26, 2017

Spika awavutia pumzi CUF

Spika wa Bunge, Job Ndugai

SIKU moja baada ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba kutangaza kuwavua uanachama wabunge wanane na madiwani mawili, Spika wa Bunge, Job Ndugai amekiri kupokea barua kuhusu uamuzi huo, na anatafakari kabla ya kutoa uamuzi.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano, Ibara ya 71 (f) chama cha siasa kina mamlaka ya kumsimamisha uanachama na hivyo anapoteza haki ya kuwa mbunge kupitia chama hicho. Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Ndugai alisema ataitafakari na kuifanyia kazi barua hiyo na ataitolea taarifa baadaye.

“Suala la kuwaondoa uanachama ni la utashi wa vyama vyenyewe, na kila chama kina utaratibu wake, hivyo bado naendelea kuitafakari barua hiyo na uamuzi kuhusu wabunge waliofukuzwa uanachama nitautolea baadaye,” alisema Spika Ndugai (pichani).

Profesa Lipumba alisema Dar es Salaam jana kuwa mbali na wabunge hao, Baraza la Uongozi la chama pia limewavua uanachama madiwani wawili wa Viti Maalumu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa makosa ya kinidhamu tangu Julai 24, mwaka huu.

Aliwataja wabunge kuwa ni Riziki Shahali Ngwali, Saverina Mwijage, Salma Mwassa, Saumu Sakala, Riziki Lulida, Mgeni Jadi Kadika, Raisa Abdallah Mussa, Miza Bakari, Halima Ali Mohammed na Khadija Al Kassim.

Madiwani waliovuliwa nyadhifa zao ni Diwani Viti Maalumu, Leila Hussein Madibi (Ubungo) na Diwani wa Viti Maalumu, Elizabeth Magwaja (Temeke). Wabunge na madiwani hao wanatuhumiwa kutokana na kitendo cha kupewa na kupokea maelekezo kutoka kwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na kula njama za kukihujumu CUF kwa kushiriki katika operesheni iliyoandaliwa na Chadema iliyoitwa ‘Ondoa Msaliti Buguruni’, jambo linalokiuka Katiba ya CUF ya 1992.

Pia wabunge na madiwani hao walikihujumu chama hicho katika uchaguzi wa marudio wa madiwani uliofanyika Januari 22, mwaka huu. Pia waliruhusu na kuipa fursa Chadema kuwa msemaji wa masuala ya CUF, kinyume cha matakwa ya Katiba yao na kulipia pango na kufungua ofisi ya chama Magomeni bila kufuata taratibu za kikatiba.

Pia inaonesha kwamba wanatuhumiwa hao, walichangia fedha zilizotumika kukodisha mabaunsa kwa lengo la kuwadhuru viongozi watiifu wa chama upande wa Lipumba, Sakaya na Mkurugenzi wa CUF wa Mambo ya Nje na Mbunge wa Mtwara Mjini, Maftaha Nachuma.

Profesa Lipumba alisema kabla ya kuvuliwa uanachama, waliitwa mbele ya Kamati ya Maadili wao waliosusia mwito huo wa kwenda kujieleza juu ya tuhuma zinazowakabili za kula njama na Chadema ili kuweza kumwondoa yeye madarakani.

Wabunge na madiwani hao walisusia mwito hata baada ya kupewa barua za kuitwa na Kamati ya Maadili, hivyo Baraza Kuu limechukua maamuzi kwa kufuata Katiba yake ya mwaka 1984 kuwafuta uanachama.

Aidha, Lipumba alisema taarifa kuhusu uamuzi huo tayari zimeshatumwa kwenda kwenda Ofisi ya Spika wa Bunge, Job Ndugai ambaye amethibitisha kuipata barua na ameahidi kuitafakari na kuitolea uamuzi baadaye na kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kwa ajili ya hatua zaidi.

Profesa Lipumba alisema wabunge 10 hao walioitwa na kuhojiwa na Kamati ya Maadili ya CUF na kugomea mwito huo ni wale wanaomuunga mkono Katibu Mkuu, Maalim Seif.

Historia ya chama hicho inaonesha kwamba hiyo si mara ya kwanza Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF, kuwafukuza wanachama kwani Januari 4, mwaka 2012, lilimfukuza uanachama aliyekuwa Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed na wenzake watatu.

Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya Mbunge huyo kuingia kwenye msuguano mkubwa na Katibu Mkuu ambaye pia wakati huo alikuwa Makamu wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi, Maalim Seif Sharif Hamad.

Hamad Rashidi baada ya kuondolewa wanachama, alisikika akisema tatizo kubwa hapa katika siasa za Kitanzania ni kwamba “viongozi wetu wa juu hawataki kupata changamoto kutoka kwa waandamizi wao kwani hawako tayari kuona mawazo kupingwa.”

Pamoja na Hamad Rashid ambaye pia alikuwa Mjumbe wa Baraza Kuu, wengine waliofukuzwa ni Doyo Hassan Doyo, Shoka Khamis Juma, Juma Said Sanani na Yasini Mrotwa.

Mbunge huyo Hamad Rashid Januari 10, 2013, na wenzake 10 waliwasilisha maombi madogo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, wakiiomba itamke kuwa uamuzi wa Baraza la Uongozi Taifa la chama hicho uliomvua uanachama yeye na wenzake ni batili na haikufanya hivyo.

No comments: