Wednesday, July 26, 2017

Wanaume Wanaoteswa na Wake Zao Lindi Wapewa Ofa

Na. Ahmad Mmow, Lindi.
JAPOKUWA shirika lisilo la kiserikali la msaada wa kisheria kwa wanawake na watoto mkoani Lindi (LIWOPAC) limejikita katika kutoa msaada wa kisheria kwa wanawake na watoto. Hata hivyo limetoa wito kwa wanaume waishio mkoani humu wanaofanyiwa vitendo vya kikatili na wakezao waende wapewe msaada wa kisheria.

Wito huo umetolewa leo na mkurugenzi wa shirika hilo, Cosma Bulu, wakati wa kongomano la wasaidizi wa utoaji wa huduma za msaada wa kisheria waliopo katika halmashauri za mkoa wa Lindi, lililofanyika mjini Nachingwea. Bulu alisema ingawa shirika lake limejikita limejikita zaidi katika kuwasaidia wanawake na watoto, lakini limeona kunaumuhimu mkubwa wa kuwasaidia hata wanaume wanaofanyiwa vitendo vya kikatili na wake zao.

Huku akibainisha kuwa wanaume wanaofanyiwa vitendo vya kikatili wapo. Bali wengi wao wanaona aibu kwenda kuwashitaki wake zao. Japokuwa kisheria zilizopo zinatakiwa kutumiwa na watu wa jinsia zote. "Sisi tunafahamu kuwa wapo wanawake wenzetu wanawanyanyasa , wanatesa na kuwafanyia ukatili. Lakini kutokana na tabia ya mfumo dume wanaona aibu kuja kuomba msaada ili wasaidiwe. Wanaona aibu," alisema Bulu.

Mkurugenzi huyo alisisitiza kwa kusema sheria zilizopo hazipo kwa ajili ya jinsia fulani,bali zote. Hivyo hata wanaume wanasitahili kusaidiwa. Ingawa waathirika wakubwa wa vitendo vya ukatili, unyanyasaji na ubaguzi ni akinamana na watoto. Alibainisha kwamba wao kama watoaji wa msaada na watetezi hawana ubaguzi katika kutoa msaada kwa mtu anae hitaji msaada wao. "Sasa tukisema hatuwasaidii wanaume sidhani kama itakuwa sawa.

Tena hawa wenzetu hawana chama wala umoja wa kutetea wanaume. Sio kama hawaonewi ila hawasemi, kuna wanawake ni wababe kwelikweli," alisisitiza na kusababisha washiriki kuangusha vicheko. Bulu alibainisha kuwa hawana uwezo wa kumfingulia mtu mashitaka, bali jukumu lao ni kutoa msaada wa kisheria.

Hasa kwa wanawake na watoto. Lakini pia kutoa elimu ili jamii iweze  kuzitambua na kudai haki za msingi za binadamu. Msaada ambao unatolewa bure bila malipo. Aidha mkurugenzi huyo alitoa wito kwa jamii kujenga tabia ya kuitafutia ufumbuzi na kumaliza migogoro yake badala ya kutegemea na kukimbilia mahakamani na kwenye mabaraza katika mambo ambayo yanaweza kusuluhishwa na jamii yenyewe kupitia vikao vya familia na ukoo. "Sasa hakuna  moto wa jioni, muda wa kukutana na kukumbushana maadili mema hakuna, ndio sababu hata uadilifu umepungua miongoni mwa jamii," alisema  Bulu. Kongamano hilo la siku mbili lililofadhiliwa na Taasisi ya huduma za uwezeshaji kisheria (LSF) lengo lake kuu ni kuimarisha upatakanaji wa haki katika jamii.

Hasa kwa wanawake na watoto kwa kuongeza ubora  na uwezo wa utoaji huduma za msaada wa kisheria. Ambapo mradi huo unatambulika kama mradi wa kuboresha huduma za upatakanaji wa huduma za kisheria. Ulioanza  mwaka jana na unatekelezwa kwa kipindi cha miaka minne.

No comments: