Sunday, September 17, 2017

Zitto Kabwe azungumzia nyumba yake kuteketea kwa moto

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe amewataka wananchi kuwa watulivu wakati Jeshi la Polisi likiendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha moto ulioteketeza nyumba yake.

Nyumba hiyo iliteketea jana Jumamosi alasiri na hakuna madhara kwa binadamu yaliyotokea isipokuwa mali zote zilizokuwamo ndani zimeteketea.

“Tumepata ajali kidogo. Nyumba yangu ninayoishi katika eneo la Kibingo, mji mdogo wa Mwandiga, Kigoma imeteketea kwa moto jioni hii. Alhamdulillah, kuwa hakuna binaadam aliyeumia,” aliandika Zitto katika ukurasa wake wa Facebook.

Alisema analishukuru Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, majirani zake na wananchi wenzake kwa ushirikiano walioutoa ili kuzima moto huo.

“Kwa sasa Jeshi la Polisi wanafanyia kazi kujua chanzo cha ajali. Naomba wananchi wawe watulivu wakati Polisi wanaendelea na uchunguzi husika,” alisema Zitto.

Nyumba hiyo aliyoijenga wakati akigombea ubunge kwa mara ya kwanza iko kiwanja kimoja na nyumba yake ya sasa.

Msaidizi wa mbunge huyo, Nyembo Mustafa alisema Zitto hakuwa anaishi kwenye nyumba hiyo baada ya kujenga nyingine kubwa kwenye kiwanja hicho.

No comments: