Monday, October 2, 2017

Maeneo yanayoongoza kwa mimba za utotoni

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Watoto wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Margaret Mussai, ameutaja Mkoa wa Katavi kuwa ndiyo unaongoza kwa kuwa na tatizo la mimba za utotoni kwa takribani asilimia 45.

Akizungumza na Wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam hivi karibuni kuhusiana na maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike yanayofanyika kila mwaka Oktoba 11, Mussai amesema Mkoa wa Katavi ndiyo unaongoza huku ukifuatiwa na Tabora 43%, Dodoma  39%, Mara 37% na Shinyanga 34% .

Mussai amesema maadhimisho ya siku hiyo kitaifa mwaka huu yatafanyika Mara kuanzia Oktoba 8, kwa kuwa mkoa huo uko ndani ya mikoa mitano nchini inayoongoza kwa tatizo hilo la mimba za utotoni.

Aidha amebainisha kwamba mgeni rasmi katika maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.

"Tunatarajia elimu itakayotolewa kupitia maadhimisho haya kwa wazazi, walezi na jamii itachangia kupunguza tatizo hili kwa kiwango fulani," amesema Mussai.

Pamoja na hayo Mkurugenzi huyo amebainsha kwamba tatizo la mimba za utotoni lipo katika jamii zote duniani na lina athari kubwa kiafya na linachangia kukatisha ndoto za maendeleo za watoto wengi wa kike.

No comments: