Thursday, December 14, 2017

Tanzania yajitenga na Trump kuhusu Jerusalem

Religious sites in Jerusalem's Old City

Haki miliki ya pichaAFP
Image captionMji wa Jerusalem una maeneo matakatifu kwa Waislamu, Wakristo na Wayahudi
Tanzania imesema haikubaliani na hatua ya Rais wa Marekani Donald Trump ya kuutambua mji wa Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel.
Wizara ya mambo ya nje ya Tanzania kupitia taarifa imesema nchi hiyo inaunga mkono makubaliano ya kimataifa ambayo yanatambua haki ya watu wa Palestina kumiliki Mashariki mwa Jerusalem kama ilivyokuwa kwenye mpaka wa kabla ya mwaka 1967.
"Tanzania inaunga mkono msimamo wa Umoja wa Mataifa wa suluhu ya mataifa mawili ambayo unatoa nafasi ya Israel na Palestina kuwepo kwa pamoja zikiwa na mipaka salama," taarifa hiyo iliyotuwa saini na Waziri Augustine Mahiga imesema.
Bw Trump kando na kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel, alisema nchi hiyo pia itahamisha ubalozi wake kutoka Tel Aviv.
Bw Mahiga amesema ubalozi wa Tanzania utaendelea kuwepo mjini Tel Aviv.
Msimamo wa Tanzania unaenda sambamba na msimamo wa mataifa mengi ya Afrika pamoja na Tume ya Umoja wa Afrika (AU).
Mwenyekiti wa tume hiyo Moussa Faki alikuwa ametahadharisha kwamba hatua ya Trump "itaongeza uhasama kanda hiyo na hata maeneo mengine na kutoa changamoto zaidi katika juhudi za kutafuta suluhu ya mzozo wa Israel na Wapalestina.
Alisema Umoja wa Afrika unaendelea kuwaunga mkono Wapalestina na juhudi zao za "haki za kuwa na taifa huru ambalo litakuwa na Jerusalem Mashariki kama mji wake mkuu."
"Hatua hii inatishia sio tu Mashariki ya Kati bali pia inachokoza ulimwengu woye wa Waislamu. Tunahofia kwamba hatua hii haitaathiri sio tu Afrika vibaya, bali pia itaifanya hali, ambayo kwa sasa inahitaji suluhu ya maiafa mawili, kuwa mbaya zaidi kuliko awali," alisema Bw Faki.
Jumatano, mataifa 57 ya Kiislamu yalitoa wito kwa Jerusalem Mashariki kutambuliwa kama mji mkuu wa Wapalestina.
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alikuwa ameyahimiza mataifa hayo katika mkutano mkuu wa muungano wa nchi za Kiislamu (OIC), kufanya hivyo akisema hatua ya Marekani ya kuutambua mji huo kama mji mkuu wa Israel ni "batili".
Bw Erdogan pia kwa mara nyingine aliishutumu Israel na kuiita "taifa la kigaidi".
KIongozi wa Wapalestina Mahmoud Abbas amesema Marekani "imejiondoa kutoka kwa kuwa mhusika mkuu katika shughuli ya kutafuta amani".
Hadhi ya mji wa Jerusalem imekuwa sehemu ya mzozo wa Waisraeli na Wapalestina.
Kwa nini Jerusalem inazozaniwa?
Mji huo una maeneo matakatifu ya dini tatu zenye kufuata imani ya Ibrahim - Uyahudi, Ukristo na Uislamu - sana maeneo mengi yanapatikana Jerusalem Mashariki.
Israel ilitwaa eneo hilo kutoka Jordan wakati wa vita kati ya nchi za Kiarabu na Israel mwaka 1967 na imekuwa ikiuchukulia mji wote kuwa mji wake mkuu ambao hauwezi kugawanywa.
Jerusalem Mashariki hutazamwa kuwa mji mkuu wa taifa la Wapalestina (litakapoundwa) na mataifa ya Kiarabu na Kiislamu pamoja na Wapalestina wenyewe.
Kwa mujibu wa maafikiano wakati wa mazungumzo ya amani ya Wapalestina na Waisraeli ya 1993, hatima ya mji huo ilifaa kuamuliwa wakati wa hatua za mwisho za mazungumzo.
Jerusalem
Hatua ya Israel kudhibiti Jerusalem yote haijawahi kutambuliwa kimataifa na nchi zote zina afisi za kibalozi Tel Aviv.
Tangu 1967, Israel imejenga makazi kadha ya Wayahudi na kuna takriban walowezi 200,000 wa Kiyahudi eneo hilo. Makazi haya yamekuwa yakishutumiwa na jamii ya kimataifa.
Kwa nini Trump akafanya hivyo?
Rais Trump alisema kwamba "ameamua ni wakati mwafaka kutambua rasmi Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel."
"Nimeamua hatua hii itakuwa ndiyo bora zaidi kwa maslahi ya Marekani katika juhudi za kutafuta amani kati ya Waisraeli na Wapalestina," alisema.
Alisema ameiagiza wizara ya mambo ya nje ya Marekani kuanza kuuhamisha ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv hadi Jerusalem.
Licha ya onyo kwamba hatua kama hiyo inaweza kuzua wimbi la machafuko kanda ya Mashariki ya Kati, hatua hiyo inatimiza ahadi aliyoitoa Trump wakati wa kampeni na pia kuwafurahisha wafuasi wenye msimamo mkali wa Bw Trump.
Jerusalem
Bw Trump alisema kutambua Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel ilikuwa "ni kutambua uhalisia tu," na akaongeza kwamba "ndiyo hatua ya busara kuichukua."
Bw Trump alisema Marekani itaendelea kuunga mkono suluhu ya mataifa mawili - taifa la Waisraeli na Wapalestina - mataifa yote yakiishi pamoja kwa amani.
Rais huyo pia alijizuia kurejelea msimamo wa Israel kwamba Jerusalem ni mji wake mkuu wa milele ambao hauwezi kugawanywa.
Wapalestina wanataka Jerusalem Mashariki iwe mji mkuu wa taifa la Wapalestina litakapoundwa.

No comments: