Monday, January 15, 2018

Watu 11 wafariki katika ajali ya gari mkoani Kagera

Watu 11 wamepoteza maisha kufuatia ajali ya gari dogo HIACE aina ya Nissan Caravan yenye namba za usajili T 542 DKE ambapo imegonga magari makubwa mawili ya mizigo katika eneo la Nyangozi kata ya Nyantakara wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera.

Kamanda wa polisi mkoa wa Kagera Augustine Ollomi amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa ajali hiyo ilitokea jana jioni ambapo gari hilo dogo la abiria lilikuwa linatokea Kakonko mkoani Kigoma kuelekea Kahama.
Kutokana na mwendokasi aliokuwa nao dereva huyo ambaye mpaka sasa hajatambuliwa jina lake aligonga magari mawili ya mizigo yenye namba za usajili T694 COX iliyokuwa ikivuta tela namba T 103 DKJ mali ya kampuni ya Mruruma Enterprises ya Dar es Salaam.

Aidha Ollomi amesema kuwa watu 9 wamefariki hapo hapo eneo la ajali, mmoja njiani akipelekwa hospitali na mwingine amepoteza maisha leo asubuhi na kuongeza kuwa majeruhi watano wanaendelea kupata matibabu katika hospitali teule ya wilaya Biharamulo.

Abiria waliokuwa katika gari dogo ni 17, kumi na mmoja wamefariki akiwemo dereva, watano wamejeruhiwa na mmoja yuko salama.

No comments: