Sunday, September 30, 2018

Polisi watakiwa kuhudhuria nyumba za Ibada ili waweze kutenda haki


Maofisa wa Polisi nchini wametakiwa kumcha Mungu na kutenga muda wao katika kuhudhuria nyumba za ibada Misikitini na Makanisani jambo ambalo litawawezesha kufanya kazi zao kwa kutenda haki kwa raia wanaowahudumia.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Simon Sirro jijini Dar es Salaam wakati alipowaongoza waombolezaji katika mazishi ya IGP Mstaafu Samwel Pundugu aliyefariki mwishoni mwa wiki na kuzikwa katika makaburi ya Kinondoni.

Kwa Upande wake Mchungaji Andrew Fabian wa kanisa la KLPT aliyeongoza ibada ya mazishi hayo amewataka wanadamu kujiandaa mapema kwa kuwa hapa duniani siyo makazi yao bali ni wapitaji tu.

Nao baadhi ya watu waliowahi kufanya kazi na marehemu wametoa wasifu wake huku wakisema alikuwa ni mtu aliyependa kazi yake na aliifanya kwa moyo kwa lengo la kuwasaidia Watanzania.

Marehemu Pundugu alizaliwa mwaka 1928 na aliteuliwa kuwa IGP mwaka 1973 hadi  mwaka 1975 ambapo pia aliwahi kuwa Mkuu wa Chuo cha Polisi Moshi CCP na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI).

No comments: