Fistula ni hali inayotokea baada ya kutokea kwa njia isiyo ya kawaida inayounganisha mfuko wa mkojo na uke kuruhusu mkojo na haja kubwa kutoka kwenye kuta za uke bila kujizuia.
Hali hii ya kushindwa kujizuia kutoa haja kubwa na ndogo hutokea baada ya mwanamke mjamzito kuwa katika hali ya uchungu wa kujifungua kwa muda mrefu kutokana na kichwa cha mtoto kushindwa kupita baada ya njia kuwa ndogo na mtoto kuwa mkubwa.
Kushindwa kupita kichwa cha mtoto na kuwa katika uchungu kwa muda mrefu husababisha tishu za uke, kibofu cha mkojo na njia ya haja kubwa kugandamizwa kati ya kichwa cha mtoto na nyonga za mwanamke hali inayosababisha ukosefu wa damu katika tishu hizi baada ya mfumo wa damu kuharibika hivyo kuziweka tishu katika mfumo ujulikanao kitaalam kama Ischemic necrosis.
Baada ya tishu kuharibiwa tundu hutokea kati ya uke na kibofu cha mkojo ama kati ya uke na njia ya haja kubwa ambapo husababisha mwanamke kutoa haja kubwa au ndogo bila kujizuia kupitia uke wake.
Taarifa kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) zinasema kuwa zaidi ya wasichana na wanawake milioni 4 ulimwenguni wanaishi na tatizo hili huku wanawake 50,000 mpaka 100,000 wakipata tatizo hili kila mwaka.
Hata hivyo pamoja na takwimu hizo ugonjwa huu umekuwa ukiripotiwa zaidi katika bara la Afrika na Asia ya Kusini ambapo kwa Tanzania takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya wanawake 1,200 hupata ugonjwa wa Fistula kila mwaka.
Tafiti zilizowahi kufanyika nchini Tanzania ziliripoti kuwa wanawake wanoathirika zaidi na ugonjwa huu ni wale wenye umri wa miaka 22 hadi 24.
Ugonjwa wa fistula husababishwa na uchungu wa muda mrefu (Prolonged and obstructed labor) ambao husababishwa na kutokuwepo kwa uwiano kati ya nyonga ya mama na ukubwa wa mtoto aliye tumboni ama mtoto kulala vibaya.
Lakini pia wataalamu wa afya wanabaini fistula mara nyingi hutokea kwa wanawake wanaojifunglia majumbani baada ya kukosa matibabu. Ni Sahihi mara kwa mara kwa wajawazito kujifungua katika kituo cha matibabu ambapo unaweza kufuatiliwa na kupata huduma za matibabu kwa wakati ni muhimu.
Mtu anapopatwa na ugonjwa huu anaweza kuugundua kwa kuona anatokwa na mkojo ama haja kubwa bila kujizuia. Hali hii inaweza kusababisha maambukizi mbalimbali ambapo mama anaweza kuanza kupata dalili za homa na maumivu ya mbavu na tumbo chini ya kitovu.
Ili kubaini ugonjwa huu kitaalamu, wataalamu wa afya huchunguza majimaji yanayotoka katika kuta za uke na mkojo ambao huoteshwa kuangalia vimelea vya ugonjwa pamoja na kujua dawa inayofaa kutibu vimelea hivyo.
Mgonjwa anaweza kutibiwa kwa kuwekewa mpira wa kukojolea kwa siku 30 endapo tatizo hili litakuwa limegundulika mapema baada ya upasuaji na kwa fistula ndogo chini ya sentimeta moja huweza kupona yenyewe au kupungua kwa kiasi kikubwa.
Endapo tatizo ni kubwa mgonjwa anaweza kufanyiwa upasuaji kulingana na mapendekezo ya daktari yatakayoendana na mahitaji ya mgonjwa.
Hivi karibuni Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, jinsia, Wazee na Watoto ilitoa tamko la wagonjwa wa fistula kutibiwa bure katika hospitali za serikali ikiwa ni juhudi zinazofanywa ili kupunguza tatizo la ugonjwa huu pamoja na kuwasaidia wanawake wengi wanaoteseka kutokana na kupata ugonjwa huu.
Swali linaweza likaja Kwenda
Je nifanye nini ikiwa nina fistula?
Kama unahisi kutokwa na mkojo bila kujizuia, harufu mbaya, maumivu makali sahemu za uzazi unashauliwa kuwahi hospitali au kituo cha afya kilichopo karibu nawe ili upate ushauri na matibabu zaidi.
Lakini kama hiyo haitoshi ni kwamba matibabu ya Fistula hutolewa bure katika hospitali ya CCBRT iliyopo jijini Dar es Salaam, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) pamoja na katika hospitali ya Rufaa ya Bugando iliyopo jijini Mwanza.
No comments:
Post a Comment