SHIRIKA la Umeme Tanzania, (TANESCO), limewaomba wateja wake na wananchi kwa ujumla kutoa taarifa mapema mara inapotokea hitilafu ya umeme iliyosababishwa na mvua au sababu nyingine.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam leo Mei 11, 2017, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka, (pichani juu), alisema, sambamba na hilo pia wananchi wasifanye shughuli au kukaa chini ya miundombinu ya umeme.
“Lakini tunawaomba wananchi watoe taarifa haraka maeneo yenye mafuriko au mkusasnyiko wa maji mengi ili wataalamu wetu waweze kuchukua hatua za haraka.” Alisema.
Dkt. Mwinuka pia alisema endapo kuna nyaya, nguzo au kifaa chochote cha umeme kimepata hitilafu na kinahatarisha maisha ni vema uangalizi au alama ikawekwa ili kuwapa hadhari wapiti njia na watoto wasikaribie eneo hilo wakati mafundi wa TANESCO wakichukua hatua za marekebisho.
Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Tanzania (TMA), katika taarifa yake iliyotoa Mei 9, 2017 imeonya kuwa maeneo ya Pwani ya Kaskazini ikiwemo visiwa vya Unguja na Pemba, yatakabiliwa na vipindi vifupi vya mvua kubwa inayozidi milimita 50 ndani ya saa 24 kuanzia Mei 10 hadi 12, 2017. Aidha kwa upande wake, mtaalamu wa masualaya umeme kutoka
TANESCO, Mhandisi Simon Kihiyo, amewahakikishia wananchi kuwa miundombinu ya TANESCO iko imara na salama, na hitilafu zinazotokea za hapa na pale nyingizinasababishwa na sababu za kibinadamu, au za kimazingira kama vile nguzo za umeme kugongwa na magari, au miti kuangukia nguzo. "Naomba nitoe angalizo kwa wateja wetu, kama pametokea hitilafu yoyote ya umeem nyumbani kwako, ni vema ukatoa taarifa TANESCO au ukamtafuta fundi wa umeme mwenye taaluma badala ya kushughulikia tatizo hilo wewe mwenyewe ilihali ukiwa huna utaalamu na masuala ya umeme, kwani hiyo ni hatari."
No comments:
Post a Comment