Friday, September 15, 2017

ATCL yapunguza hasara kwa bilioni 17/-

Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi

KAMPUNI ya Ndege Tanzania (ATCL), imepunguza hasara kwa kiasi kikubwa kutoka Sh bilioni 20 hadi kufi kia Sh bilioni 3 kwa mwaka.

Hayo yamebainishwa jana mjini hapa na Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi aliyeeleza kuwa katika mpango wao wa muda mfupi ambao ni wa mwaka mmoja, wamefanikiwakupunguza hasara kwa kiasi hicho. Matindi alisema kufanikiwa huko kumetokana na kufanyika kazi katika baadhi ya maeneo ambayo yalikuwa ni changamoto ikiwemo ufutaji wa safari, akieleza kuwa awali walikuwa wakifuta safari, lakini kwa sasa hawafuti safari.

Pia kumekuwapo na udhibiti wa mapato. Alisema wamejiwekea Mpango Mkakati wa Biashara wa muda mrefu ambao ni wa miaka mitano na kwamba una malengo matatu ikiwemo usalama, kuhakikisha wanatengeneza faida pamoja na kutoa huduma zenye uhakika kwa wateja wao. Aidha, alisema wamejiwekea tathmini ikiwa ni pamoja na kuangalia mambo ambayo ni hatari na jinsi ya kukabiliana nayo.

ATCL kwa sasa inamiliki ndege mbili aina ya Bombardier Q400 zinazotoa huduma katika sehemu mbalimbali nchini ambazo zimenunuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano ambazo kwa kiasi kikubwa zimesaidia kulirejesha shirika hilo katika usafiri wa anga. Ndege nyingine inatarajiwa baadaye mwaka huu. Naye Katibu wa Baraza la Wafanyakazi la ATCL, Margret Leslie alisema lengo la kuwepo kwa baraza hilo ni kuwakutanisha wafanyakazi na menejimenti ili kupanga maendeleo na matarajio yao ya baadaye.

Kwa upande wake, Mwezeshaji wa mafunzo, Ofisa Elimu Kazi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na wenye Ulemavu, Emmy Rweyendela alisema baraza la wafanyakazi ni chombo cha mawasiliano ya kazi kinachowaunganisha wafanyakazi na uongozi katika kutoa ushauri na majadiliano katika kuzungumzia mpango kazi na uchumi wa taasisi kwa kutathimini juu ya ufanisi na tija ili malengo yaliyokusudiwa yatimizwe.

No comments: