Sunday, September 17, 2017

Polisi Dsm anayejiita 'Faru John' atakiwa kuhojiwa


Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amemuagiza Kaimu Kamanda wa Mkoa wa Temeke kuhakikisha askari anayejiita Faru John anafikishwa ofisi kwake kuhojiwa akituhumiwa kwa rushwa.

Agizo hilo amelitoa leo Jumapili baada ya wakazi wa Mbagala kumlalamikia wakidai askari huyo amekuwa akiwakamata wafanyabiashara na kudai kwa nguvu rushwa ya Sh20,000.

Wananchi  hao wamelalamika kuwa, mfanyabiashara ambaye hatoi fedha hizo hufungwa pingu na kuzungushwa usiku kucha akiwa kwenye gari la polisi.

Kamanda Mambosasa aliyekuwa akisikiliza kero za wananchi wa Mbagala Zakhem amesema Jeshi la Polisi haliwezi kuwa na askari anayejipa jina la mzaha, huku akiwakandamiza wananchi.

Amesema huo ni mmomonyoko wa maadili kwa askari ambao kazi yao ni kulinda raia na mali zao, hivyo atawachukulia hatua wote watakaobainika kuomba na kupokea rushwa.

"Ninawaomba askari kuwalinda wafanyabiashara wenye mitaji midogo kama vile wakaanga chipsi. Kuwadai Sh20,000 eti kwa sababu wamechelewa kufunga biashara hilo sikubaliani nalo hata kidogo, lazima niwachukulie hatua," amesema Kamanda Mambosasa.

Pia, amekemea askari wanaodai rushwa kwenye vituo vya polisi ambavyo amesema vipo kwa ajili ya kutoa huduma.

Amewaagiza wakuu wa vituo kuhakikisha watu hawakai muda mrefu vituoni kwa kuwa kufanya hivyo ni kutengeneza mazingira ya kupokea rushwa.

Mkazi wa Mbagala, Thabiti Mohamed alisema kuna askari anayejulikana kwa jina la Faru John amekuwa akiwakamata wafanyabiashara, wakiwemo wauza chipsi ambao huchelewa kufunga maduka hadi saa tano usiku na huzunguka nao usiku kucha wakiwa wamewafunga pingu.

Mohamed alisema askari hao huomba kwanza Sh20,000 ili kuwaachia na wasipozitoa ndipo hufungwa pingu na kupakiwa kwenye gari.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Kibangulile, Mashaka Selemani amemuomba Kamanda Mambosasa kuwahamisha askari wa Kituo cha Polisi Maturubai akisema hawakamati wahalifu bali wapo kwa ajili ya kupokea rushwa.

"Askari hawa kazi yao wanapomkamata mtuhumiwa wanampeleka ofisi ya Serikali ya Mtaa Mikwambe, wanapofika kazi yao wanataka fedha kwa nguvu. Wasipopata wanawapiga na kuwabambikia kesi. Tumefuatilia wanakusanya hadi Sh1 milioni kwa siku, hivyo wameshazoeleka tunataka waondolewe Mbagala," alisema Selemani.

No comments: