Monday, September 25, 2017

Upinzani kuandamana Kenya

Viongozi wa upinzani nchini Kenya Kalonzo Musyoka, Raila Odinga na Musalia Mudavadi

Image captionVinara wa upinzani Kenya Kalonzo Musyoka, Raila Odinga na Musalia Mudavadi
Chama cha upinzani nchini Kenya NASA kimeitisha maandamano Jumanne nje ya makao makuu ya tume ya uchaguzi IEBC mjini Nairobi.
Hatua hii ni ya kushinikiza kujiuzulu kwa baadhi ya maafisa wa juu wa tume hiyo walioshiriki kuandaa uchaguzi mkuu wa August 8 mwaka huu uliobatilishwa na mahakama ya juu nchini.
NASA umeeleza kwamba hautovamia makao ya tume ya IEBC kama ilivyotajwa awali kuwatimua kwa lazima maafisa hao, badala yake unasema maandamano yatakuwa ya amani katika barabara za mji mkuu Nairobi kushinikiza kujiuzulu kwao.
Hilo ni mojawapo ya masharti iliyotoa NASA kushiriki uchaguzi wa marudio uliotangazwa kufanyika Oktoba 26 mwaka huu.
Rais Uhuru Kenyatta ametoa onyo kwa wapinzani ambao amesema watakumbana na mkono wa sheria iwapo maandamano yao yataingilia shughuli za kiuchumi za raia wa nchi hiyo.
Rais Uhuru Kenyatta ameuonya upinzani kuwa watakumbana na mkono wa sheria iwapo maandamano yatakumbwa na ghasia
Image captionRais Uhuru Kenyatta ameuonya upinzani kuwa watakumbana na mkono wa sheria iwapo maandamano yatakumbwa na ghasia
Amesema, 'Endeleeni na maandamano yenu, mukigusa mboga za mama wanaouza barabarani, tuko na nyinyi. Mukigusa maduka ya watu tuko na nyinyi. Lakini kama hamuna lingine lolote la kufanya isipokuwa kutembea - tembeeni. Mimi nawaambia hata mukinitukana mpaka asubuhi, haitabadilisha dunia'.
Upinzani unasisitiza kuwa una haki ya kuandamana kwani hata upande wa serikali - Muungano wa Jubilee - umeshafanya maandamano kama hayo hivi juzi walipoelekea katika mahakama ya juu zaidi wakitaka majaji wa mahakama hiyo waondolewe.
Mmoja ya vinara waandamizi wa kambi ya upinzani, Musalia Mudavadi ameiambia BBC, kuwa mahakama ya juu zaidi ilisema IEBC ilishindwa kuandaa uchaguzi mkuu kulingana na sheria.
Ameeleza, 'Tume ya IEBC sio vyombo tu, bali ina watu ndani ambao ni maafisa wanaohudumu katika kitengo cha usajili wa watu, masuala ya teknolojia ya mawasiliano na kadhalika, walishindwa kutekeleza wajibu wao na ndio wanaoweza kuondolewa.
Muungano wa NASA unataka jumla ya maafisa 12 wa tume hiyo washtakiwe kwa kutowajibika katika uchaguzi uliobatilishwa wa Agosti 8.
Unataka pia mfumo wa teknolojia uliotumiwa wakati wa uchaguzi huo ubadilishwe.

No comments: