Thursday, September 28, 2017

Wakamatwa kwa kuuza mbolea bei tofauti na bei elekezi ya serikali.

Mamlaka ya udhibiti wa mbolea Tanzania TFRA imeanza operesheni maalum kuwakamata na kuwachukulia hatua wamiliki wa maduka ya pembejeo za mifugo wanaouza mbolea bei juu ikilinganishwa na bei elekezi iliyotolewa na serikali ambapo mkoani Morogoro maduka kadhaa yamefungiwa na wamiliki pamoja na wafanyakazi wake kutiwa mbaroni na jeshi la polisi.

Bei elekezi ya mbolea ya shilingi 37,000 ile ya kukuzia ya Urea na 50,000 kwa DAP ya kupandia, ilitolewa na waziri wa kilimo,mifugo na uvuvi Dkt. Charles Tizeba kuanzia agosti 18 mwaka huu, baada ya kukutana  na kufanya mazungumzo baina ya Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli na mfalme wa Morroco aliyekuja nchini,ambapo bei hiyo ilipunguzwa kufikia asilimia 34 hadi kufika bandarini,lakini bado baadhi ya wafanyabiashara wamedaiwa kukiuka na kuuza Urea kwa shilingi 50,000 na DAP ikikosekana madukani.

Kwa mujibu wa mkaguzi huyo wa mbolea,kukamatwa kwa watu hao kunatokana na kukiuka kwa ibara ya 40 ya sheria ya mbolea ya mwaka 2009 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2014 ambapo mfanyabiashara yeyote atakayeuza mbolea zaidi ya bei elekezi atatozwa faini ya papo hapo ya shilingi milioni 80 au kifungo kisichozidi miaka mitatu au adhabu zote kwa pamoja.

Hata hivyo waliokamatwa katika zoezi hilo kwa kuuza mbolea kwa bei juu walikataa kuzungumza lolote kuhusiana na operesheni hiyo,huku wenye maduka mengine ya pembejeo waliokataa kupigwa picha wakidai bei hiyo ya juu inatokana na manunuzi toka jijini Dar es Salaam.

No comments: