Sunday, October 1, 2017

Serikali imesema Tanzania hupoteza dola Milioni 350 kwenye hili


Waziri wa Maliasili na utalii Mheshimiwa Jumanne Maghembe ameiomba Benki kuu ya Tanzania kuhuisha mfumo wa ubadilishanaji fedha kwa njia ya kielektroniki (credit cards) ili kuchochea ukuaji wa sekta ya utalii nchini.

Waziri Maghembe ametoa ombi hilo mjini Iringa wakati akizindua maonesho ya utalii yanayoenda sambamba na maonesho ya bidhaa za wajasiliamali Kanda ya Nyanda za juu Kusini ambapo ameongeza kuwa Tanzania inakosa dola Milioni 350 kutokana na matumizi ya fedha tasilimu badala ya kadi za kielektroniki.

Aidha Waziri Maghembe ameongeza kuwa pamoja na changamoto mbalimbali ikiwemo miundombinu ya viwanja vya ndege na barabara hasa katika ukanda wa nyanda za juu Kusini bado kumekuwa na ongezeko la watalii na kuifanya sekta hiyo kuendelea kuongoza katika uingizaji wa fedha za kigeni huku mkuu wa mkoa wa Iringa Bi Amina masenza akiwataka wawekezaji kuwekeza katika sekta ya utalii kwenye eneo la nyanda za juu Kusini.

Kwa upande wake Mkurugenzi mkuu wa Shirika la kuhudumia viwanda vidogo nchini SIDO Mhandisi Profesa Sylvester Mpanduji amewataka watanzania kupenda bidhaa za nyumbani na kuzitumia badala ya utamaduni uliozoeleka wa kupenda bidhaa zinazotoka nje ya nchi.

Maonesho ya utalii na bidhaa za wajasiliamali yanafanyika katika viwanja vya kichangani kihesa mjini Iringa yakilenga kutangaza vivutio vya utalii na kuamsha ari ya uwekezaji katika sekta ya utalii katika ukanda wa nyanda za juu Kusini eneo linalotajwa kujaaliwa vivutio vingi vya utalii lakini likishindwa kupata mapato mengi yatokanayo na sekta hiyo kutokana na uduni wa miundombinu na pia vivutio hivyo kutotangazwa vyakutosha.

No comments: