Sunday, June 17, 2018

KIVUKO KIPYA 'MV MWANZA' CHASHUSHWA ZIWA VICTORIA

Mwonekano wa kivuko cha MV Mwanza baada ya kushushwa majini, Ziwa Victoria 


Mkuu wa Mkoa Mwanza, Mhe.John Mongella akizungumza baada ya MV.Mwanza kushushwa majin

Serikali imekamilisha ujenzi wa kivuko kipya na cha kisasa cha Mv Mwanza chenye uwezo wa kubeba tani 250 sawa na abiria elfu moja na magari madogo 36 kitakachotoa huduma kati ya eneo la Kigongo na Busisi katika ziwa Victoria mkoani Mwanza ambacho kimegharimu zaidi ya shilingi bilioni 8 na milioni 800.

Akiongea baada ya kushuhudia hatua ya uingizaji majini wa kivuko hicho kilichojengwa na kampuni ya kizalendo ya Songoro Marine Transport ya jijini Mwanza, Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongela amesema kivuko hicho ambacho ni mradi wa serikali kitasaidia kupunguza changamoto za usafiri katika ziwa Victoria na pia usafiri na usafirishaji kwa nchi za maziwa makuu.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa huduma za vivuko na ukodishaji wa mitambo kutoka TEMESA injinia Lukombe King'ombe amesema ujenzi wa kivuko hicho umekamilika kwa wakati kutokana na uwezo wa mkandarasi licha ya kwamba vifaa vingi vilivyotumika kujenga kivuko hicho vimeagizwa kutoka nje ya nchi.

Naye Mkurugenzi wa kampuni ya Songoro Marine Transport ya jijini Mwanza Major Songoro amesema kivuko hicho kimejengwa kwa kutumia wataalam wa ndani ambao wamefundishwa na kuwa na ujuzi mkubwa katika uundaji wa vyombo vya usafiri wa majini huku akisisitisa umuhimu wa kutumia usafiri wa majini ili kurahisisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya wananchi.

No comments: