Kufuatia wanafunzi zaidi ya 20,000 kukosa nafasi za kujiunga na kidato cha tano kwa mwaka 2018, serikali imetoa sh.bilioni 29 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo madarasa na mabweni huku waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Suleiman Jafo akitoa maagizo kwa wakuu wa mikoa kukamilisha ujenzi wa miundombinu katika mikoa yao ndani ya kipindi cha miezi miwili.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Waziri Jafo amesema wanafunzi 21,808 walikosa nafasi ya kujiunga licha ya kuwa na sifa stahiki na hali hiyo imetokana na ufaulu kuongezeka na kuwataka wakuu wa mikoa kusimamia miundombinu na thamani ya fedha kwenye miradi ionekane.
Aidha katika hatua nyingine Jafo amewataka wakurugenzi wa halmashauri nchini kuhakikisha hawakwamishi ujenzi huo na ufanyike kwa ubora unaotakiwa kwani ni azma ya serikali kuhakikisha inatoa elimu bora kwa wananchi.
Baadhi ya wakazi mkoani Dodoma wamesema ujenzi wa miundombinu hiyo utasaidia kuokoa idadi kubwa ya wanafunzi ambao wamekuwa wakikosa shule kutokana na upungufu wa miundombinu ya madarasa pamoja na Mabweni.

No comments:
Post a Comment