Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya Tarime inayomilikiwa na Halmashauri ya Mji wa Tarime mkoani Mara na watumishi watatu wa hosptalini hapo wamesimamishwa kazi baada ya gari la wagonjwa kukamatwa na mirungi
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime Elias Ntiruhungwa amewasimamisha kazi watumishi watatu akiwamo Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Tarime baada ya gari la wagonjwa la Hospitali hiyo kukamatwa likisafirisha madawa ya kulevia aina ya mirungi.
Waliosimamishwa kazi ni Kaimu Mganga Mkuu (TMO) Dk. Innocent Kweka, Kaimu Mganga Mfawidhi Dk. Amir Kombo na katibu wa Hospitali Rwegasira Karugwa ambapo awali mkurugenzi alikuwa amemchukulia hatua dereva wa gari hilo na kumsimamisha kazi, George Matai.
“Namsimamisha kazi TMO, Mganga Mfawidhi na Katibu wa hospitali kuanzia leo hadi tuakapomaliza uchunguzi wetu ambao umeanza kubaini kwa nini gari la wagojnwa lilitumika kusafirisha madawa ya kulevia .Kama hawana hatia watarudi kazini”, Mkurugenzi huyo alisema jana(Alhamisi) mchana wakati akitangaza hatua ambazo anaendelea kuchukua baada ya tukio hilo kutokea mapema wiki hii.
Ntiruhungwa alisema hawezi kuvumilia kitendo hicho amabacho kimechafua jina la Hamashauri yake na nchi kwa ujumla na kwamba yeyote ambaye atabainika kuhusika katika tukio hilo atachukuliwa hatua kali.
Alisema tayari suala hilo linafanyiwa uchunguzi wa kina ili kubaini dereva huyo George Matai alipataje fursa ya kusafirisha madawa ya kulevia kwa kutumia gari la wagonjwa.
Alisema pamoja na kwamba dereva huyo yuko mikononi mwa jeshi la polisi akisubiri kufikishwa mahakamni amesimamishwa kazi pia.
“ Yule dereva yeye tunamsimamisha kazi na akimalizana na polisi na mahakama akirudi tunamfukuza kazi wakati huohuo . Hatuwezi kuvumilia kitendo cha aibu kama hiki. Alichokifanya ni kitendo cha kusikitisha . Ni tamaa na mmomonyoko wa madili ", aliongeza Ntiruhungwa.
Mkurugenzi huyo aliwataka wakuu wa idara katika Halmashauri yake kutimiza wajibu wao kikamilifu ili kuepekuka vitendo vya aibu kama hivyo kutokea tena.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara (RPC) Juma Ndaki aliwaambia waandishi wa habari juzi kuwa dereva huyo na mtuhumiwa mwingine wanashikiliwa baada ya kukamatwa na shehena ya mirungi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Mara Adamu Kigoma Malima amewataka watumishi kufanya kazi kwa weredi huku wakizingatia taratibu za sheria za utumishi wa umma.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa Mara, Samweli Keboye alisema kuwa tukio la gari kufanya kazi za kusafirisha madawa ya kulevya badala ya kazi ya serikali ni kitendo chja kujumu wananchi.

No comments:
Post a Comment