Tuesday, August 28, 2018

Mama Samia ahudhuria kuapishwa kwa majaji Arusha


Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan amehudhuria  hafla ya kuapishwa kwa Majaji wateule watatu wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu.

Katika hafla hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Mahakama ya  Afrika  mkoani Arusha mapema Agosti 27, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Jaji Imani Aboud naye ameapishwa kuwa Jaji wa Mahakama hiyo.

Majaji wengine wawili ambao ni Jaji Blaise Tchikaya kutoka Kongo na Jaji Stella Isibhakhonem Anukam  kutoka  Nigeria. Majaji hawa watatu wameapishwa baada ya baadhi ya waliokuwa Majaji wa Mahakama ya Afrika kuachia nafasi zao kwa sababu mbalimbali.

Hafla hiyo ya kuwaapisha ilihudhuriwa na wageni mbalimbali wa Serikali ikiwa ni pamoja na Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Augustine Mahiga, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Mrisho Gambo na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mhe. Gabriel Daghalo.

Awali; Rais wa Mahakama  ya  Afrika, Mhe. Jaji Sylvain Ore alielezea kuwa baada ya uapisho huo idadi ya  Majaji wanawake katika Mahakama ya Afrika itaongezeka kutoka nne na kuwa sita.

“Kwakuwa kati ya Majaji watatu wanaoapishwa wawili ni wanawake. Kutakuwa na jumla ya Majaji kumi na moja ambao watano ni wanaume na sita ni wanawake,” alisema Jaji Ore.

Pia alisisitiza umuhimu wa mahakama hiyo katika kutetea haki za binadamu.

Baada ya ufunguzi huo,  majaji wapya walipata nafasi ya kuapa mbele ya Majaji wa Afrika,Viongozi wa Serikali, Watumishi wa Mahakama Tanzania na wageni waalikwa waliohudhuria halfa hiyo.

Kwa upande wake mgeni rasmi Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu alipopata nafasi  ya
kuzungumza aliwashukuru Majaji wa Afrika kwa mwaliko pia alipokea salamu za pole kwa niaba ya Mhe. Rais wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli.

Pia alielezea juu ya ushiriki wa nchi kuhusiana na masuala ya haki za binadamu na pia aliahidi ushirikiano wa hali ya juu kwa sababu Mahakama hiyo ya Afrika ipo katika mipaka ya nchi yake jijini Arusha.

No comments: