Tuesday, September 11, 2018

Mtumishi chuoni alipwa mishahara hewa miezi 11

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dk. Laurean Ndumbaro.

KATIBU Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dk. Laurean Ndumbaro, amemwagiza Mkuu wa Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo, Dk. Mpamila Madale,-

kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi waliohusika kumlipa mishahara hewa kwa miezi 11 aliyekuwa Mhasibu Msaidizi wa Chuo hicho, Calvin Mushi na kumpa ruhusa ya kuhamia kituo kingine cha kazi bila idhini ya Katibu Mkuu Utumishi.

Dk. Ndumbaro alitoa maagizo hayo jana baada ya kufanya ziara ya kikazi ya kushtukiza katika chuo hicho kwa lengo la kubaini sababu za kuendelea kumlipa mshahara mtumishi huyo.

Dk. Ndumbaro aliwataja watumishi wanaotakiwa kuchukuliwa hatua kuwa ni pamoja na Mkuu wa Idara ya Utumishi na Utawala wa Chuo hicho na Ofisa Utumishi anayeshughulika na Mfumo Shirikishi wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara.

Alifafanua kuwa watumishi hao wamehusika kuiletea hasara serikali kwa kumlipa mshahara mtumishi asiyestahili ambaye amehamia Bohari Kuu ya Dawa (MSD) bila idhini ya mwenye mamlaka ambaye ni Katibu Mkuu Utumishi.

Aidha, Dk. Ndumbaro amemwagiza Mkuu huyo wa Chuo kumfukuza kazi na kumfungulia mashtaka ya kinidhamu Mushi kwa kupokea mshahara katika vituo viwili vya kazi yaani Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo na Bohari Kuu ya Dawa (MSD), huku akijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.

“Kwa kuzingatia Schedule A, Ndugu Calvin Mushi asimamishwe kazi na kufunguliwa mashtaka ya kinidhamu na fedha zote alizochukua zirejeshwe serikalini,” Dk. Ndumbaro alisisitiza.

Aidha, alitoa wito kwa watumishi wote wa umma nchini kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya utumishi wa umma, ili kuunga mkono jitihada za serikali za kuwaondoa watumishi hewa kwa lengo la kuokoa fedha za serikali ambazo zingetumika katika shughuli mbalimbali za maendeleo.

Alisema Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora inaendelea kutekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhakikisha watumishi wa umma wanaolipwa mishahara wanakuwa na sifa stahiki kwa mujibu wa sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya utumishi wa umma iliyopo.

No comments: