Waandishi wa habari wakimsikiliza kwa makin mzee Nyambo hayupo pichani |
TUKIO la kuuawa kwa mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni
cha Channel ten mkoani Iringa, Daud Mwangosi, limeendelea kuibua mambo mapya,
baada ya aliyekuwa mgombea wa ubunge wa jimbo la Njombe Magharibi kupitia Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kudai chama chake kilishiriki mauaji hayo
kwa asilimia 50 na asilimia nyingine 50 ilifanikishwa na Serikali kupitia Jeshi
la Polisi.
Nyimbo alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na wandishi wa
Habari Jijini Mbeya katika mkutano wake aliouandaa kwa nia ya kutangaza nia
yake ya kujiuzulu uanachama wa Chadema na kubakia mwanasiasa huru asiye na
chama.
Alisema kuwa Chadema hawakuwa na sababu ya kwenda kuzindua tawi
la chama hicho katika kijiji cha Nyololo wilayani Mufindi kwa sababu tawi hilo
alikuwa tayari alishalizindua yeye mwenyewe miezi mitatu kabla ya kutokea kwa
mauaji ya marehemu Mwangosi.
“Asilimia hamsini, mauaji ya rafiki yangu Marehemu Mwangosi
yalisababishwa na Chadema kwa kutotii amri ya Jeshi la Polisi na kupanga kwenda
kuzindua tawi la chama ambalo mimi nikuwa tayari nimekwishalizindua miezi
mitatu iliyopita kabla ya tukio lile,” alisema Nyimbo.
Nyimbo alisema kuwa tabia ya viongozi wa kitaifa wa Chadema
kutoka makao makuu ya Chama Jijini Dar es Salaam na kwenda mikoani kufanya
mikutano ambayo huwa haijafanyiwa maandalizi yoyote na wenyeji wao, hali ambayo
inawafanya walazimike kufanya maandalizi wao wenyewe, ndiyo inayosababisha
migongano isiyokuwa ya lazima na Jeshi la Polisi na hatimaye kuwa chanzo cha
vurugu kwenye mikutano ya chama hicho.
Alisema kuwa kwa kawaida mikutano ya siasa inapaswa kuandaliwa
na wenyeji kwa kuwa ndio ambao wanaofahamiana vizuri na uongozi wa Jeshi la
Polisi katika eneo husika kwa kuwa wao wakikaa na kuzungumza huelewana, lakini
suala hilo linapoingiliwa na wageni husababisha viongozi wa sehemu husika kuwa
na wasiwasi wa usalama na hivyo kutokea migongano inayosababisha kutokea kwa
vurugu.
Akizungumzia ushiriki wa Jeshi la Polisi katika mauaji ya
Mwangosi, Nyimbo alisema kuwa haikuwa sahihi kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Iringa (RPC), Michael Kamuhanda kuingilia kati suala hilo kwa kuwa sheria ya
mikusanyiko inaeleza wazi kuwa mwenye jukumu hilo ni Mkuu wa Polisi wa eneo
linalofanyika tukio ambaye alipaswa kuwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD).
Alisema kuwa ikitokea OCD akazidiwa nguvu au kushindwa kutoa
maamuzi kwa suala husika ndipo hulazimika kuomba msaada kwa bosi wake ambaye ni
RPC ambaye naye anastahili kutoa maelekezo na sio kwenda moja kwa moja kwenye
eneo la tukio kama alivyofanya Kamuhanda.
Kwa mujibu wa Nyimbo, hata tume iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi kuchunguza chanzo cha mauaji hayo ilikuwa
ni batiri kwa sababu Dk. Nchimbi ni sehemu ya watuhumiwa kwa upande wa
Serikali.
Alisema kilichotakiwa kufanyika baada ya kutokea kwa tukio hilo
ilikuwa ni uwakamata viongozi wote wa Chadema na viongozi wa Polisi waliokuwa
eneo la tukio na kuwaweka ndani kwa muda kupisha uchunguzi wa tukio hilo na pia
kuwapa fundisho wasijaribu kuchezea roho za watanzania na amani ya taifa.
Mwangosi ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wandishi wa
Habari mkoani Iringa (IPC) aliuawa kwa kulipuliwa na kitu kinachodaiwa kuwa ni
bomu wakati akiwa kazini katika kijiji cha Nyororo wilayani Mufindi ambako
Chadema walikuwa wakizindua tawi la chama hicho kijiji hapo.
picha na mbeyayetu
No comments:
Post a Comment