PAMOJA NA UMILIKI WA KAMPUNI YA IPTL
1. KWA KUWA, Taarifa Maalum ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu
za Serikali Kuhusu Ukaguzi Maalum wa Malipo yaliyofanyika katika Akaunti
ya Escrow ya Tegeta uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (‘CAG’) pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(‘TAKUKURU’) imeonesha kwamba kwamba Harbinder Singh Sethi, James
Rugemalira (VIP), Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Waziri wa
Nishati na Madini, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wajumbe wa Bodi ya
Wakurugenzi wa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (‘TANESCO’) walihusika
kwa namna moja au nyingine katika kufanikisha kufanyika miamala haramu
ya fedha za Akaunti ya Escrow ya Tegeta kwenda kwa makampuni ya Pan
African Power Solutions Ltd. (‘PAP’), na VIP Engineering & Marketing
(‘VIP’)
KWA KUWA, kwa sababu ya kuhusika kwa watu hao na
miamala iliyofanyika kwenye Akaunti ya Escrow imeliingizia Taifa hasara
ya mabilioni ya fedha za umma zinazotokana na kutokulipwa kwa kodi mbali
mbali za Serikali na kushindwa kwa TANESCO kukokotoa upya kiwango cha
malipo ya gharama za uwekezaji (‘capacity charges’) wa IPTL;
KWA
KUWA, mabilioni ya fedha yaliyotolewa kwenye Akaunti ya Escrow
yametumika kuwapa kile kinachoonekana kuwa ni rushwa baadhi ya viongozi
na maafisa wa serikali kama vile Mawaziri, Majaji, Wabunge, Wenyeviti wa
Kamati za Bunge, wakuu wa taasisi za umma, viongozi wa dini, mawakili
wa kujitegemea na watu binafsi.
NA KWA KUWA, vitendo
vilivyofanywa na watu hawa vinaashiria makosa mbali mbali ya jinai kama
vile uzembe, wizi, ubadhirifu, kutakatisha fedha haramu, matumizi mabaya
ya madaraka, rushwa na kupokea mali ya wizi;
HIVYO BASI, BUNGE
LINAAZIMIA KWAMBA, TAKUKURU, Jeshi la Polisi na vyombo vingine husika
vya ulinzi na usalama viwachukulie hatua stahiki za kisheria, kwa mujibu
wa sheria za nchi yetu, watu wote waliotajwa na Taarifa Maalum ya
Kamati kuhusika na vitendo vyote vya kijinai kuhusiana na miamala ya
Akaunti ya Escrow, na watu wengine watakaogundulika kuhusika katika
vitendo hivyo vya jinai kufuatia uchunguzi mbali mbali unaoendelea;
2. KWA KUWA, vitendo vya kijinai wanavyhohusishwa navyo viongozi wa
umma na maafisa wa ngazi za juu serikalini vinakiuka pia maadili ya
viongozi wa umma na kuwanyima viongozi na maafisa hao uhalali wa
kuendelea kushikilia nafasi za mamlaka katika uongozi wa umma;
HIVYO BASI, BUNGE LINAAZIMIA KWAMBA, Waziri wa Nishati na Madini, Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na Wajumbe wa Bodi ya
Wakurugenzi wa TANESCO wawajibishwe, kwa kuishauri mamlaka yao ya uteuzi
kutengua uteuzi wao;
3. KWA KUWA, katika watu walioshiriki
kwa namna moja au nyingine katika kashfa ya miamala ya Akaunti ya Escrow
wapo pia viongozi wa Kamati za Kudumu za Bunge kama vile Mwenyekiti wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Nishati na Madini na ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya
Wakurugenzi wa TANESCO;
NA KWA KUWA, Bunge na/au Kamati zake za
Kudumu zina uwezo na mamlaka, kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge,
ya kuwawajibisha viongozi hawa wa Kamati kwa kuwavua nyadhifa zao;
HIVYO BASI, BUNGE LINAAZIMIA KWAMBA, Kamati husika za Kudumu za Bunge
zichukue hatua za haraka, na kwa vyovyote vile kabla ya Mkutano wa Kumi
na Nane wa Bunge, kuwavua nyadhifa zao Wenyeviti tajwa wa Kamati husika
za Kudumu za Bunge;
4. KWA KUWA, Taarifa Maalum ya Kamati
imeonesha kwamba katika watu waliotajwa kuhusika kwa namna moja au
nyingine katika kashfa ya miamala ya Akaunti ya Escrow wapo pia Majaji
wa Mahakama Kuu ya Tanzania;
KWA KUWA, Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, 1977 (‘Katiba’) imeweka utaratibu mahsusi wa
kushughulikia nidhamu ya Majaji;
KWA KUWA, utaratibu wa
kushughulikia nidhamu ya Majaji kwa mujibu wa Katiba unamtaka Rais
kuunda Tume ya Uchunguzi ya Kijaji kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili
dhidi ya Majaji;
NA KWA KUWA, utaratibu wa kushughulikia nidhamu
ya Majaji kwa mujibu wa Katiba unamruhusu Rais kumsimamisha kazi Jaji
au Majaji husika wakati uchunguzi wa tuhuma dhidi yake unaendelea;
HIVYO BASI, BUNGE LINAAZIMIA KWAMBA, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania aunde Tume ya Kijaji ya Uchunguzi kuchunguza tuhuma za utovu wa
maadili dhidi ya Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa
wa Mahakama Kuu ya Tanzania;
5. KWA KUWA, Taarifa Maalum ya
Kamati imeonesha kwamba Stanbic Bank (Tanzania) Ltd. ilishiriki kupokea
na kutakatisha fedha zilizotolewa kwa njia haramu kutoka katika Akaunti
ya Escrow na kupelekwa katika akaunti zilizofunguliwa na PAP katika
benki hiyo;
KWA KUWA, Taarifa Maalum ya Kamati imeonesha kwamba
akaunti za PAP katika Stanbic Bank Tanzania Ltd. zimekwishafungwa
baada ya fedha zote zilizotolewa katika Akaunti ya Escrow kumalizika na
Akaunti ya ya VIP katika Mkombozi Commercial Bank imebakiza kiasi fulani
cha fedha;
NA KWA KUWA, Taarifa Maalum ya Kamati inaonesha
kwamba kuna uwezekano fedha zilizotolewa kutoka kwenye akaunti za PAP na
VIP zilipelekwa katika benki nyingine;
NA KWA KUWA, vitendo vya
Stanbic Bank (Tanzania) Ltd., na benki nyingine kupokea na kutakatisha
fedha zilizotolewa kwenye Akaunti ya Escrow ni vitendo vya jinai kwa
mujibu wa Sheria ya Udhibiti wa Fedha Haramu;
HIVYO BASI, BUNGE
LINAAZIMIA KWAMBA, mamlaka husika za kifedha na za kiuchunguzi ziitaje
Stanbic Bank (Tanzania) Ltd. na benki nyingine yoyote itakayogundulika,
kufuatia uchunguzi wa mamlaka za kiuchunguzi, kujihusisha na
utakatishaji wa fedha zilizotolewa katika Akaunti ya Escrow, kuwa ni
taasisi zenye shaka ya utakatishaji wa fedha haramu (institutions of
money laundering concern);
6. KWA KUWA, vitendo vya wizi,
ubadhirifu wa mali ya umma, hujuma ya uchumi na ufisadi vimeongezeka,
kushamiri na kushirikisha viongozi wa kisiasa na maafisa wa serikali
pamoja na wafanya biashara wakubwa;
KWA KUWA, kwa mujibu wa
sheria iliyoiunda, TAKUKURU inashughulikia vitendo vya aina zote za
rushwa zikiwemo rushwa ndogo ndogo (petty corruption) na rushwa kubwa na
ufisadi (grand corruption) na matumizi mabaya ya madaraka;
NA
KWA KUWA, kwa sababu ya majukumu yake mapana kisheria, TAKUKURU
inaelekea kuelemewa katika vita ya kupambana na kudhibiti vitendo vya
rushwa kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa taifa
letu kiuchumi, kijamii na kisiasa;
HIVYO BASI, BUNGE LINAAZIMIA
KWAMBA, Serikali iandae na kuwasilisha Muswada wa marekebisho ya Sheria
iliyoiunda TAKUKURU kwa lengo la kuanzisha taasisi mahsusi
itakayoshughulikia, kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa,
ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa taifa kiuchumi, kijamii
na kisiasa;
7. KWA KUWA, Taarifa Maalum ya Kamati imeonesha
jinsi ambavyo TANESCO imekuwa ikitumia mabilioni ya fedha kulipa gharama
za umeme unaozalishwa na IPTL na hivyo kuathiri hali ya kifedha ya
Shirika hilo;
KWA KUWA, Taarifa Maalum ya Kamati inaonesha kwamba
TANESCO itaendelea kulipa fedha nyingi kwa ajili ya gharama za umeme
huo wa IPTL;
HIVYO BASI, Bunge linaazimia kwamba Serikali
iangalie uwezekano wa kununua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na
kuimilikisha kwa TANESCO kwa lengo la kuokoa fedha za Shirika hilo.
8. KWA KUWA, kwa miaka mingi mikataba mibovu ya kuzalisha umeme kati
ya TANESCO na makampuni binafsi ya kufua umeme imeisababishia TANESCO
hasara ya mabilioni ya fedha na hivyo kutishia uhai wake wa kifedha;
KWA KUWA, Bunge lilikwishaazimia kwamba serikali iwasilishe mikataba
husika Bungeni au kwenye Kamati zake kwa lengo la kuliwezesha Bunge
kutekeleza vyema wajibu wake wa kuisimamia na kuishauri serikali;
NA KWA KUWA, Serikali haijatekeleza Azimio hilo la Bunge hadi sasa;
HIVYO BASI, Bunge linaazimia kwamba Serikali itekeleze Azimio husika la
Bunge mapema iwezekanavyo na kwa vyovyote vile kabla ya kumalizika kwa
Mkutano wa Bunge la Bajeti Serikali iwasilishe taarifa ya utekelezaji wa
mapitio ya mikataba ya umeme.
Imewasilishwa leo hii tarehe 28 Novemba, 2014.
------------------------------------------------------
ZITTO ZUBERI KABWE (MB)
MWENYEKITI
KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI
No comments:
Post a Comment