Serikali imesema kuwa VICOBA ni
taasisi binafsi inayomilikiwa na wananchi wenyewe vikiwa ni miongoni mwa
tasisi ndogo za kifedha ambazo ni za kibinafsi na huanzishwa,
kuendeshwa na kusimamiwa ama kijijini, kitongojini na hata kwenye kata.
Hayo yamebainishwa leo Bungeni
mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba alipokuwa akijibu
swali la Mbunge wa Rungwe Magharibi Prof. David Mwakyusa (CCM) ambaye
alitaka kujua kama Serikali inatambua VICOBA kama mkombozi wa wanyonge.
Mwigulu amefafanua kuwa taasisi hizo zimo kwenye sekta ya fedha isiyorasmi na zinatoa huduma za kifedha mijini na vijijini.
“Uwepo wa taasisi hizi,
umewezesha kufikisha huduma za kifedha kwa wananchi waliombali na huduma
za sekta rasmi ya fedha na hivyo kuwa mkombozi wa wanyonge” alisema
mwigulu.
Aidha, kwa kutambua suala hilo,
ili kusaidia na kuimarisha taasisi hizo, Mwigulu amesema kuwa Serikali
baada ya kupata ushauri kutoka kwa Mshauri Mwelekezi wa masuala ya
uchumi na tafiti za kijamii, inafanya mapitio ya Sera ya Taifa ya
Taasisi ndogo za huduma ya fedha ya mwaka 2000 ili kuihuisha iweze
kukabili na kuzingatia mabadiliko na maendeleo yanayojitokeza katika
sekta hiyo.
Vilevile Mwigulu amesema kuwa
Serikali inakamilisha uhuishaji wa sera ya taasisi ndogo ndogo za
kifedha ambapo hatua inayofuata ni kuandaa mapendekezo ya muswada ambayo
yatapelekwa Baraza la Mawaziri mara baada ya kupata idhini na maelekezo
ya Baraza hilo na muswada huo utafikishwa bungeni.
Taasisi ya VICOBA ilianzishwa
nchini mwanzoni mwa miaka ya 2000, ambapo imekuwa na manufaa kwa
wananchi wengi wenye kipato cha chini hususan wanawake waishio vijijini
wamefanikiwa kuboresha kipato chao na maisha yao kwa ujumla kwa kujiunga
na taasisi hiyo.
No comments:
Post a Comment