Mkuu
wa Bandari ya Kigoma, Bw. Athuman Malibamba (Kulia) akimkaribisha
Kiongozi wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais,
Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri (Kushoto) mara alipofika kujionea
maendeleo ya bandari hiyo.
Mkuu
wa Bandari ya Kigoma, Bw. Athuman Malibamba (Katikati mbele) akifafanua
jambo kwa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais,
Tume ya Mipango mara walipofika kujionea shughuli za maendeleo kiwanjani
hapo.
Mratibu
wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya
Mipango, Bw. Senya Tuni (Wapili kushoto) akiuliza jambo kwa Mkuu wa
Bandari ya Kigoma, Bw. Athuman Malibamba (Wapili kulia) walipofanya
ziara bandarini hapo.
Mkuu
wa Bandari ya Kigoma, Bw. Athuman Malibamba (Wapili kulia) akifafanua
jambo kwa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais,
Tume ya Mipango mara walipofika kujionea shughuli za maendeleo kiwanjani
hapo.
Afisa
utekelezaji wa Bandari Kigoma, Bw. Teophil Luoga (Kulia aliyechuchumaa)
akiwaonesha eneo la upanuzi wajumbe wa timu ya Ukaguzi wa Miradi ya
Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango mara walipofika kujionea
shughuli za maendeleo kiwanjani hapo.
Boti na meli zikipandisha shehena kwenye Bandari ya Kigoma.
PICHA ZOTE NA SAIDI MKABAKULI
…………………………………………………………………………………………
Na Saidi Mkabakuli, Kigoma
Serikali imeazimia kuendelea
kuboresha miundombinu ya bandari hususan miradi iliyoibuliwa katika
Programu ya Matokeo Makubwa Sasa ikiwemo kuanza kufanya upanuzi wa
Bandari ya Kigoma na kuendelea kuboresha miundombinu na ununuzi wa
vifaa mbalimbali vya kuhudumia shehena katika Bandari ya Kigoma ili
kuweza kukidhi mahitaji yanaongeza siku baada ya siku katika bandari
hiyo.
Ahadi hiyo imetolewa na Kiongozi
wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya
Mipango, Bibi Florence Mwanri wakati walipofanya ziara ya kukagua
maendeleo ya miundombinu katika Bandari ya Kigoma.
Bibi Mwanri alisema kuwa serikali
kupitia Mamlaka ya Bandari nchini nchini ipo kwenye mkakati wa
kuiendeleza bandari hiyo ili iwe ya kiwango kizuri kwa kuhudumia
watumiaji wa wa bandari hiyo.
“Kama munavyokumbuka Serikali
katika mwaka huu wa fedha ilipanga kuiendeleza na kuboresha miundombinu
ya usafiri wa majini na anga ili kuongeza ufanisi wa sekta hizi, ambapo
Bandari ya Kigoma ni mojawapo ya bandari zilizopewa kipaumbele kwa ajili
ya uendelezaji,” alisema Bibi Mwanri.
Kwa mujibu wa Bibi Mwanri, upanuzi
wa bandari hiyo upo kwenye hatua za upembuzi yakinifu kwa ajili ya
kuboresha bandari ya Kigoma na kutwaa maeneo zaidi kwa ajili ya upanuzi
wa bandari hiyo.
Akitoa taarifa ya maendeleo ya
Bandari hiyo, Mkuu wa Bandari hiyo Bw. Athuman Malibamba alisema kuwa
mpaka kufikia Juni 2014 hatua ya utekelezaji iliyofikiwa ni kukamilika
kwa kazi ya uthamini wa mali eneo la Kibirizi lenye hekta 10 kwa ajili
ya upanuzi wa bandari hiyo. “Pia, Mamlaka imempata Mtaalam Mshauri (M/S
Royal Haskoning H.D.V Nederland, B.V) atakaefanya kazi ya Upembuzi
Yakinifu. Aidha, kazi ya uthamini wa mali imekamilika kwa eneo la
Katosho lenye hekta 69 kwa ajili ya kujenga bandari kavu,” alisema.
Kuongezeka kwa shughuli za
kiuchumi katika nchi za jirani kunatoa fursa ya kuimarisha miundombinu
ya bandari ya Kigoma ili kuwa na uwezo wa kuhudumia shehena
inayoongezeka na kukuza uchumi katika mkoa na Taifa kwa ujumla. Aidha
kuanzishwa kwa Eneo Maalum la Kiuchumi, katika mkoa wa Kigoma ni
kichocheo muhimu kwa Mamlaka ya Bandari (TPA) kuimarisha huduma katika
bandari ya Kigoma na hivyo kuweza kuzitumia fursa zitakazojitokeza mara
baada ya shughuli mbalimbali za kiuchumi kuanzishwa.
No comments:
Post a Comment