Tunapoelekea kipindi hiki cha
uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ambao unatarajiwa kufanyika tarehe 14
Disemba, 2014, kwa taarifa tulizonazo, katika baadhi ya maeneo hapa
nchini, kumejitokeza makundi ya vijana wanaopita katika baadhi ya maeneo
na kuwatishia watu waliojiandikisha kupiga kura hususani wazee na
wanawake kuwa, siku ya kupiga kura wasijitokeze na endapo watajitokeza
watafanyiwa vurugu.
Jeshi la Polisi nchini, linatoa
onyo kali kwa mtu yeyote au kikundi chochote cha watu kutokujihusisha na
vitendo vya vurugu, fujo ama vitisho vinavyoweza kusababisha uvunjifu
wa amani wakati wa zoezi zima la uchaguzi wa viongozi wa Serikali za
Mitaa.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi katika
mikoa yote limejipanga vizuri kwa kushirikiana na vyombo vingine vya
ulinzi na usalama kuhakikisha kwamba hakuna vitendo vyovyote vya
uvunjifu wa amani vitakavyojitokeza wakati wa kampeni na hata siku ya
kupiga kura na pale ambapo vitajitokeza vitadhibitiwa kwa haraka, na
wahusika kukamatwa.
Aidha, Jeshi la Polisi nchini,
linawatoa hofu wananchi wote kwamba, ulinzi umeimarishwa katika maeneo
yote kipindi hiki chote cha kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa na
hata siku ya upigaji kura. Waliojiandikisha kupiga kura wote wajitokeze
siku ya kupiga kura bila hofu ya aina yoyote.
Jeshi la Polisi linaendelea kuomba
ushirikiano wa jamii kutoa taarifa za mtu ama vikundi vya aina yoyote
vinavyojihusisha na vitendo vya vitisho, vurugu na fujo dhidi ya
wananchi waliojiandikisha kupiga kura ili hatua kali za kisheria ziweze
kuchukuliwa dhidi yao mapema.
Imetolewa na:-
Advera John Bulimba – SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.
Advera John Bulimba – SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.
No comments:
Post a Comment