Rais Xi Jinping wa China, ameridhia ombi la Rais John Magufuli la nchi hiyo kutoa ufadhili wa masomo kwa madaktari 20 wa Tanzania.
Taarifa iliyotolewa leo Jumatatu Agosti 6, 2018 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa imesema madaktari hao watasomea shahada ya uzamili na uzamivu katika matibabu ya ini na uboho kwenye Chuo Kikuu cha Shandong nchini humo.
Katika taarifa hiyo imeelezwa kuwa leo balozi wa China nchini, Wang Ke amewasilisha ujumbe huo kwa Rais Magufuli sambamba na kutoa nafasi 30 za wataalam watakaohudhuria semina ya mafunzo ya usimamizi wa hospitali.
Rais Magufuli alitoa ombi hilo Novemba mwaka jana wakati meli ya matibabu kutoka China ilipowasili nchini kwa ajili ya kuwafanyia vipimo na kutoa tiba kwa watu waliokuwa na magonjwa mbalimbali.
Wakati huo huo, Rais Magufuli ameagana na Balozi wa Canada hapa nchini Mhe. Ian Myles na Balozi wa Ubelgiji hapa nchini Mhe. Paul Cartier baada ya Mabalozi hao kumaliza muda wao.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akiagana na balozi wa Canada nchini aliyemaliza muda wake Mhe. Ian Myles walipokutana Ikulu jijini Dar es salaam leo Agosti 6, 2018.
Baada ya mazungumzo hayo Mabalozi hao wameelezea kufurahishwa kwao na uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na nchi zao na wamempongeza Rais Magufuli na serikali anayoiongoza kwa hatua kubwa za kuleta mageuzi ya kiuchumi, kuboresha utendaji kazi wa watumishi wa umma, kupambana na rushwa na kuboresha huduma za kijamii.
No comments:
Post a Comment