Wednesday, August 29, 2018

Serikali kuajiri askari 1500, Kangi Lugola anena


Serikali imetenga zaidi ya shilingi Bilioni 4.5 kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa mwaka wa fedha 2018/2019 na kuajiri askari wapya 1500 ili kuongeza nguvu kazi ya jeshi hilo ili liweze kutoa huduma zitakazokidhi viwango vya kitaifa na kimatafa katika kuelekea kwenye mapinduzi makubwa ya uchumi wa kilimo na viwanda.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi Kangi Lugola amesema mikakati hiyo ya serikali kwenye uzinduzi wa wiki ya zimamoto na uokoaji inayoadhimishwa kwa mara ya kwanza nchini ambapo anasema kutokana na kukua kwa uchumi na teknolojia taifa linapaswa kujiandaa katika kukabiliana kikamilifu na majanga ikiwemo ya ajali na moto.

Aidha Waziri Kangi ameliagiza Jeshi la Zimamoto na uokoaji kushirikiana na halmashauri zote hasa za miji inayokuwa katika kuandaa ramani za mipango miji ili kuweka mazingira rafiki na miundombinu ya kukabiliana na majanga ikiwemo ya moto.

Awali katika Maadhimisho hayo Kamishna Jenerali wa Jeshi la zimamoto na uokoaji Thobias Andengenye amesema jeshi hilo limeendelea kuboresha huduma kwa jamii licha ya kukabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo uhaba watumishi vifaa duni vya kuzimia moto huku akiitaka serikali kusaidia kuzitatua.

Kwa upande wao wadau na wananachi waliohudhuria Maadhimisho hayo wamesema imefika wakati sasa jamii kuwa na uelewa mpana juu ya kukabiliana na majanga hasa katika kipindi hiki cha ulimwengu wa mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia na tabia nchi.

No comments: