
Polisi nchini Afrika kusini wamethibitisha vifo vya watu wawili katika mapigano yaliyotokea kati ya wenyeji na wageni katika mji wa Soweto.
Katika ghasia hizo maduka yanayomilikiwa na wageni yaliporwa bidhaa, wakati vurugu zilipotapakaa eneo lote.
Ghasia za kupinga wahamiaji zimekuwa zikijitokeza nchini Afrika kusini, hali inayosababishwa na tatizo kubwa la ukosefu wa ajira na umasikini.
Vurugu zinazochochea uporaji wa vitu zimesambaa katika maeneo mengi ya Soweto.
zilianzia katika duka moja, baada ya wakazi wa eneo hilo kumtuhumu mmiliki wa duka mwenye asili ya Somalia kumshambulia kwa risasi na kumuua kijana mdogo aliyedai kuwa alikuwa akijaribu kuvunja duka lake.
Polisi nchini humo wana amini kwamba tukio hilo ndio lililozua mtafaruku na kusababisha ghasia ambazo sasa zimesambaa katika maeneo kadhaa ya mji huo.
Wakazi hao pia wanawalaumu wamiliki wa maduka, ambao wengi ni wageni, kuuza vyakula vilivyopitwa na wakati.

Ujumbe wa WhatsApp umekuwa ukizunguuka nchini Afrika kusini ukimuonya yeyote yule, aliyepangisha vyumba kwa Wasomali, awafukuza.
Kwa mujibu wa ujumbe huo iwapo hawatafanya hivyo mpaka ifikapo tarehe 8 Septemba nyumba zote na maduka yatachomwa moto.
Idadi ya maduka haya yanayomilikiwa na wageni yamejengwa katika maeneo ya karibu na makazi na yamekuwa yakimilikiwa raia pia kutoka nchi nyingine kama vile Ethiopia, Zimbabwe na Pakistan.
Hali hiyo pia imewafanya wamiliki wengi wa maduka kufungasha bidhaa zao na kuondoka mjini humo wakihofia vurugu zaidi.
No comments:
Post a Comment