Thursday, December 27, 2012

Maamuzi Ya Baraza La Madaktari Juu Ya Madaktari Waliogoma


 UTANGULIZI

Kutokana na mgomo wa madaktari uliotokea kati ya tarehe 23 na 29 mwezi

juni 2012.Wizara iliwasilisha malalamiko kwenye Baraza la madaktari
Tanganyika ili lifanye uchunguzi kuhusu madaktari hao .Idadi ya
madaktari wote waliogoma walikuwa 394, kati yao madaktari 376 walikuwa
ni madaktari walio katika mafunzo kwa vitendo (Interns) kutoka
hospitali za Muhimbili, K.C.M.C. Bugando, Mbeya Rufaa, St.Francis -
Ifakara, Dodoma, Temeke, Mwananyamala, Amana, Haydom na Sekou Toure.
Aidha, Madaktari waajiriwa(Registrar) 18 walishiriki katika mgomo huo
kutoka hospitali ya Rufaa ya Mbeya.
Baraza lilipitia malalamiko yote na limetoa adhabu stahiki kwa kila

daktari aliyethibitishwa kushiriki katika mgomo huo.  Adhabu hizo
zilikuwa katika makundi yafuatayo; onyo, onyo kali na kusimamishwa
udaktari kwa muda wa kati ya mwezi mmoja na miezi sita.Vile vile kuna
Madaktari ambao hawakuwa na hatia ya kushiriki katika mgomo na hivyo
walifutiwa mashtaka.

MCHANGANUO WA ADHABU

•       Waliofutiwa mashitaka madaktari 49

•       Waliopewa onyo  madaktari 223
•       Waliopewa onyo kali madaktari 66
•       Kusimamishwa kwa muda madaktari 30
•       Mashitaka yaliyoahirishwa kutokana na wahusika kuhitaji ushauri wa
kisheria madaktari 4
•       Mashitaka yasiyosikilizwa kutokana na wahusika kutofika walipoitwa
na Baraza madaktari 22
Wizara inakamilisha taratibu za kinidhamu kwa mujibu wa Kanuni za

Utumishi wa Umma kwa Madaktari wote waajiriwa ambao walipatikana na
hatia mbele ya Baraza la Madaktari.   Wizara pia imeridhia kuwapa
Madaktari waliokuwa katika mafunzo kwa vitendo fursa nyingine ya
kuendelea na mafunzo hayo katika hospitali za Umma walizokuwepo kabla
ya kuondolewa.  Hata hivyo fursa hii haitawahusu Madaktari wote
waliopewa adhabu za kusimamishwa na Baraza la Madaktari, hadi hapo
watakapomaliza kutumikia adhabu zao.
HITIMISHO

Kwa taarifa hii madaktari wote waliofutiwa mashtaka na wale waliopewa
onyo na onyo kali wanatakiwa kuwasilisha kwa Katibu Mkuu Wizara ya
Afya na Ustawi wa Jamii barua kutoka kwa msajili wa Baraza la
Madaktari ikithibitisha kurejeshewa usajili  na kuruhusiwa kuendelea
na mafunzo kwa vitendo. Vile vile madaktari waajiriwa(Registrar)
wanatakiwa pia kuripoti kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya ili kupewa
barua zao kulingana na Adhabu walizopewa.  Barua hizi zitatolewa
kuanzia tarehe 2 Januari, 2013.Madaktari wote walio katika mafunzo kwa
vitendo wanatakiwa kuanza kazi katika vituo vyao vya awali  ifikapo
tarehe 14 Januari, 2013.Hakuna muda utakaoongezwa kwa kipindi
kilichobakia cha mafunzo kwa vitendo. Kwa wale wote waliopewa adhabu
wataanza kutumikia adhabu hizo kuanzia tarehe ya adhabu hiyo
ilivyotolewa.
Nsachris Mwamwaja

Msemaji
WIZARA YA AFYA NA USTAWI  WA JAMII
27/12/2012
 

Hukumu Kesi Ya Lema Yaibua Mapya


 Na: James Magai

MWANAZUONI aliyebobea katika sheria, Profesa Issa Shivji na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Francis Stolla wamekosoa hukumu ya Mahakama ya Rufani, iliyomrejesha bungeni, Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti juzi, wanasheria hao walisema hukumu hiyo iliyotolewa na majaji watatu wakiongozwa na Nathalia Kimaro, Salum Massati na Bernard Luanda, inapingana na sheria.

Hata hivyo, mmoja wa mawakili wa Lema, Method Kimomogoro amepinga madai hayo akisema wanaoipinga pengine hawajapata nafasi ya kuliangalia kwa undani suala la haki ya mpiga kura kupinga matokeo mahakamani.

Profesa Shivji kwa upande wake alieleza kushangazwa na maelezo ya Mahakama ya Rufani kuwa mpiga kura hana haki ya kufungua kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi na kusema hiyo ni sawa na kutunga sheria mpya na si kutafsiri zilizopo.


Alisema Sheria ya Bunge ya Uchaguzi, Katiba ya nchi na Mahakama, vinampa haki mpiga kura kufungua kesi kupinga matokeo ya uchaguzi.

“Sheria ya Bunge na Mahakama Kuu katika kesi ya Mgonja (Chediel ya mwaka 1980), vinampa haki mpiga kura kufungua kesi mahakamani kupinga matokeo. Sijaona hoja nzito ya Mahakama ya kufuta haki hiyo ya mpiga kura,” alisema Profesa Shivji.

Katika shauri hilo namba 84 la mwaka 1980 lililofunguliwa na William Bakari na mwenzake dhidi ya Mgonja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Mahakama Kuu Tanzania iliamua kuwa, mpiga kura ana haki kufungua kesi mahakamani kupinga matokeo. Walalamikaji walishinda.

Hata hivyo, Mahakama ya Rufani katika kesi ya Lema, iliamua kwamba hukumu katika kesi ya Mgonja ilikosewa kwani si sahihi kwamba mtu yeyote bila kujali mahali alipojiandikisha na kupiga kura anaweza kupinga matokeo katika jimbo lolote nchini hata kama haki zake hazijakiukwa kwa namna yoyote.

Lakini Profesa Shivji aliitetea hukumu hiyo ya Mgonja akisema imekuwapo kwa zaidi ya miaka 30 sasa na kwamba kwa muda wote huo imekuwa ikifuatwa katika uamuzi wa mashauri mbalimbali, huku akisisitiza kuwa Mahakama haiwezi kuifuta kirahisi tu.

Profesa Shivji alisema mpiga kura ni mwananchi na kwa vyovyote ana masilahi katika uchaguzi husika na hivyo anatarajia kuona uchaguzi ambao ni huru na wa haki.
“Hivyo huwezi kusema hahusiki na nani kashinda au kashindwa kwa kuwa uchaguzi ni muhimu katika kujenga na kukuza demokrasia,” alisema Profesa Shivji.

Chama cha Wanasheria
Kwa upande wake, Stolla alisema: “Nimesikiliza hata maoni ya wanasheria mbalimbali wakizungumzia kutofurahishwa na tafsiri ya Mahakama ya Rufani kuhusu haki ya mpiga kura ‘ku-challenge’ (kupinga) matokeo ya uchaguzi mahakamani,” alisema na kuongeza:


“Katika uamuzi wa kisheria, inaonekana Mahakama imetunga sheria mpya na wengi tunajiuliza kama siyo, sababu ya kuwa mpiga kura ni ipi nyingine inampa haki mpiga kura kupinga matokeo?”

Stolla alisema Sheria ya Bunge ya Uchaguzi ya tangu mwaka 1985, ambayo ilifanyiwa marekebisho mwaka 2002, kabla ya kutungwa upya mwaka 2005, inampa haki mpiga kura kupinga matokeo ya uchaguzi mahakamani.

“Mwaka 2002, sheria zote zilifanyiwa marekebisho na baadaye mwaka 2005, Bunge likatunga sheria mpya inayoitwa Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, ikafuta ya mwaka 1985. Sheria hiyo na marekebisho yake, ndiyo inayotawala uchaguzi hadi sasa,” alisema.

Alisema hata kabla ya kutungwa kwa sheria hiyo ya Uchaguzi ya mwaka 1985, tayari kulikuwa na uamuzi wa Mahakama Kuu katika kesi ya Mgonja ambayo iliamua kuwa mpiga kura ana haki ya kupinga matokeo ya uchaguzi mahakamani.
NA
 Umoja Wa Makanisa Nchini Kuliombea Taifa Disemba 31 Uwanja Wa Taifa


MUUNGANO wa Makanisa nchini unatarajia kufanya Mkesha wa kuliombea Taifa ili amani na utulivu uliopo uweze kudumu, ambao unatarajiwa kufanyika Desemba 31 mwaka huu kwenye viwanja vya Taifa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na wandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, Godfrey Malassy , alisema mkesha huo umekuwa ukifanyika kila Desemba 31 ya kila mwaka, kuukaribisha mwaka mpya.
 
Alisema lengo la mkesha huo ni kuliombea Taifa hilo mungu, ili aweze kuliponya na kulinusuru na majanga mbalimbali, na kudumisha amani miongoni mwa jamii yote nchini.
 
Malassy aliongeza kuwa Taifa kwa sasa linapita katika kipindi kigumu hususani kuanzia uelewa, uchumi, na katika masuala ya usalama wa raia wa ndani na nje ya nchi ambapo kuna baadhi ya watu wameanza kuichezea amani kwa kusababisha vurugu kwa kvisingizio vya dini.
 
Pia alisema kuwa Watanzania wanapaswa kudumisha amani na utulivu kwani hiyo ni tunu ambaayo wamepatiwa na mungu hivyo haipaswi kuchezewa na watu wachache wasio na nia njema.
 
“Mkesha wa dua hilo, utafanyika Desemba 31 mwaka huu kuanzia saa 2:00 usiku hadi asubuhi katika viwanja vya Taifa Dar es Salaam, na tunatarajia Rais Jakaya Kikwete atakuwa mmoja wa wageni wetu waalikwa” alisema Malassy.
 
Malassy alibainisha kuwa mkesha huo wa maombezi utashirikisha mikoa zaidi ya 16 ya Tanzania Bra na Visiwani, ambapo utakuwa na lengo la kuwaleta Watanzania kuliombea Taifa kwa ajili ya kudumisha amani, umoja na mshikamano visitetereke.

No comments: