Friday, January 9, 2015

MFUMUKO WA BEI NCHINI WAENDELEA KUPUNGUA

Displaying Takwimu - 1.jpg
Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Ephraimu Kwesigabo akitoa taarifa ya kupungua kwa mfumuko wa bei nchini kwa mwezi Desemba, 2014 leo jijini Dar es salaam.Wengine ni Meneja wa Takwimu za Ajira na Bei wa Ofisi hiyo Bi. Ruth Minja (kushoto) na Johnson Nyella, Meneja Utafiti wa Uchumi wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT).

Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Desemba 2014 umepungua hadi kufikia asilimia 4.8 kutoka asilimia 5.8 iliyokuwepo mwezi Novemba kutokana na kupungua kwa bei ya bidhaa na huduma katika maeneo mbalimbali nchini.

Akitoa taarifa ya Mfumuko wa Bei wa Taifa leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Bw. Ephraim Kwesigabo amesema kuwa kupungua kwa bei za bidhaa za vyakula zikiwemo Mahindi, Unga wa mahindi, mbogamboga, mihogo ,sukari ,Mafuta ya taa, dizeli, petroli na Simu za kiganjani kumechangia kupunguza mfumuko wa bei nchini.
Amesema kuwa wastani wa Mfumuko wa Bei wa Taifa wa mwaka mzima kutoka Januari hadi Desemba 2014 umepungua hadi kufikia asilimia 6.1 kutoka asilimia 7.9 uliokuwepo kuanzia Januari hadi Desemba mwaka 2013.

Ameeleza kuwa Tanzania inaendelea kufanya Vizuri katika nchi za Afrika Mashariki katika kudhibiti Mfumuko wa bei kwa kuendelea kuchukua hatua za kudhibiti viashiria vinawezakuchangia kuwepo kwa mfumuko wa bei.
Akitoa ufafanuzi kuhusu mfumuko wa bei katika baadhi ya nchi za Afrika Mashariki Kwesigabo amesema kuwa umekuwa na mwelekeo unaofanana, Kenya ukipungua na kufikia asilimia 6.02 mwezi Desemba kutoka 6.09 za mwezi Novemba na Uganda ikiwa na mfumuko wa bei wa asilimia 1.8 kutoka asilimia 2.1 za mwezi Novemba, 2014.

Aidha, amesema mwenendo wa Fahirisi za bei ambacho ni kipimo kinachotumika kupima mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zinazotumiwa na kaya nchini katika kipindi cha mwezi Desemba 2014 amesema kuwa Fahirisi hizo zimeonyesha kuongezeka hadi kufikia150.92 kutoka 150.54 za mwezi Novemba 2014.
Amefafanua kuwa kuongezeka kwa Fahirisi hizo kunatokana na kuongezeka kwa bei za bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula zikiwemo mchele, unga wa mahindi, samaki, matunda jamii ya machungwa, mbogamboga, mavazi ya wanaume na wanawake na viatu vya wanaume.
Kwa upande wake Meneja Utafiti wa Uchumi wa Benki Kuu ya Tanzania Bw. Johnson Nyella ameeleza kuwa kuendelea kupungua kwa Mfumuko wa Bei nchini kunatokana na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali kupitia Benki hiyo kwa kuangalia utekelezaji wa Sera na Mipango ya maendeleo.
Amesema kuwa katika kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kuwa na utulivu wa Uchumi kwa kipindi kirefu, Benki Kuu ya Tanzania imekuwa ikifuatilia mwenendo wa bei katika Soko la Dunia, bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini na ufuatiliaji wa mwenendo wa uchumi wa nchi zinazoizunguka Tanzania.
Amesema malengo ya muda mrefu ya Benki kuu ya Tanzania ni kuhakikisha kuwa Mfumuko wa bei unapungua na kufikia asulimia 5.
MWISHO.

No comments: